Maafisa elimu Kata 136 mkoani Singida wamepatiwa mafunzo maalumu kuhusu Usimamizi Saidizi katika maeneo yao ya uongozi wa shule na ujazaji wa takwimu katika Mfumo wa "School Information System" (SIS). Mafunzo hayo yamefanyika Machi 24,2025 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, yakihudhuriwa na viongozi wa elimu ngazi ya Mkoa, Wathibiti Ubora wa shule Mkoa na Wilaya, Wakuu wa Divisheni Elimu ya Awali na Msingi, yakiongozwa na wawezeshaji kutoka ADEM na TAMISEMI.
Akifungua mafunzo kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Elipidius Baganda amepongeza juhudi za maafisa elimu Kata katika kutekeleza majukumu yao, akibainisha kuimarika kwa ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya taifa. Aidha, ameutambua mchango wa Mradi wa Shule Bora katika kuboresha ufundishaji wa walimu na ujifunzaji kwa wanafunzi wote wakiwemo wenye mahitaji maalumu kutokana na weledi wa walimu kupitia mafunzo mbalimbali yanayofanyika katika halmashauri zote za mkoa wa Singida. Na amewasihi wadau wa elimu kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha elimu kwa ngazi zote, ikiwemo elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi.
"Mafunzo haya yanalenga kuwaongezea ujuzi maafisaelimu Kata ili waweze kusimamia ipasavyo shughuli za elimu katika maeneo yao, hususani katika kuhakikisha ujazaji sahihi wa taarifa za shule kwenye Mfumo wa SIS." alisema Dkt. Baganda
Pia, Amesisitiza umuhimu wa kuongeza ufaulu wa wanafunzi, kukamilisha miundombinu kwa ubora, kutoa taarifa za maendeleo kila wiki, huku akiwakumbusha watumishi wa umma kutojihusisha na siasa.
"Hakikisheni ufaulu wa wanafunzi unaongezeka, miundombinu ya shule inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, taarifa za maendeleo zinatolewa kila mwisho wa wiki. Pia, ni muhimu mtumishi wa umma kuepuka kujihusisha na masuala ya kisiasa, ili kuepusha mgongano wa maslahi." alisema Dkt. Baganda
Shule Bora ni mradi wa Serikali unoatekelezwa kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na TAMISEMI, ukisimamiwa na Cambridge Education kama mshauri na kufadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia FCDO.
No comments:
Post a Comment