Friday, September 13, 2024

VIJANA WALEMAVU WAPEWE RUHUSA YA KUSHIRIKI MAENDELEO KATIKA JAMII.


Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe ametoa wito kwa jamii kuwapa vipaumbele vijana na watoto wenye ulemavu kushiriki shughuli mbalimbali katika jamii kwani wakipewa nafasi wengi wana uthubutu na vipaji vingi vyenye tija katika kuchangia ukuaji wa uchumi na maendeleo makubwa katika jamii na nchi yetu kwa ujumla.

Mhe. Gondwe ameyasema hayo (Septemba 12, 2024) alipotembelea banda la chuo cha ufundi na marekebisho kwa watu wenye ulemavu Saba Saba, katika maonyesho yanayoendelea Mkoani Singida ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji wananchi kiuchumi ambapo chuo hicho kina wanafunzi wengi wenye ulemavu tofauti tofauti ikiwemo wasioona, viziwi, ulemavu wa viungo, ulemavu wa ubongo, na  ulemavu wa afya ya akili wanaojishuhulisha na sanaa mbali mbali ikiwemo mafunzo ya umeme, ushonaji, uokaji, mapambo, useremala na uchomeleaji.

"Serikali imeaandaa nazingira mazuri sana kwa watu wenye mahitaji maalum, matokeo yake ni haya yanayoonekana hapa kwa vijana hawa waliojifunza na kupata ujuzi wa mambo mbalimbali, hivyo kila mzazi ampe mtoto au kijana wake nafasi ya fursa katika jamii na fursa za mafunzo mbalimbali" alisema Mhe. Gondwe.

Hosea, mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo, ni mwanafunzi wa mwaka wa pili chuoni hapo anayesoma masomo ya ushonaji katika chuo cha ufundi na marekebisho kwa watu wenye ulemavu Sabasaba, ametoa rai kwa jamii kwa kuepuka kuwatenga, kuwaficha ndani na kuwanyima fursa walemavu kwa kuhofia mchango duni kutoka kwao waachane na mila hiyo na kuwapa nafasi kwani wana mchango mkubwa sana katika kuchangia maendeleo.

"Jamii isituone sisi kama walemavu, sisi ni vijana imara na tunaweza kufanya mengi makubwa kama watu wasio walemavu, wazazi wasiwafiche watoto ndani kwasababu ni walemavu, watupe nafasi na ruhusa ya kushiriki  mambo mbalimbali katika jamii". Alisema Hosea

Maonyesho hayo ya mifuko na program za uwezeshaji wananchi kiuchumi kilele chake ni tarehe 14 Septemba, 2024 Mkoani humo ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu Dotto Biteko.



No comments:

Post a Comment