Friday, September 13, 2024

TAKUKURU WATOA ELIMU KWA WAPIGA KURA NA WAGOMBEA KATIKA UCHAGUZI.

Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe. Godwin Gondwe ametoa wito kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuendelea kutoa elimu kwa wapiga kura, wagombea na wananchi kwa ujumla juu ya majukumu ya taasisi hiyo kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka  2024.

Gondwe ameyasema hayo (Septemba 12, 2024) wakati akitembelea mabanda katika maonyesho ya mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi yanayoendelea mkoani Singida katika viwanja vya Bombadia.

"Natoa wito kwa taasisi ya TAKUKURU, kushauri vijana kuhusu suala la uchaguzi na kutoa elimu kwa wapiga kura na wagombea wote juu ya kazi na ushiriki wa taasisi hiyo hasa katika uchaguzi ujao" alisema Gondwe.

Kwa upande wao Taasisi ya Uuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeazimia kuendelea kutoa elimu juu ya rushwa kuendelea kwa kuwashauri vijana, na wananchi wote kwa ujumla kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa 2024.

TAKUKURU wamesema wanaendelea kutoa huduma kwa kuhakikisha wanazidi kuhamasisha na kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya rushwa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi serikali za mitaa 2024 kwa dhumuni kubwa la kuhakikisha uchaguzi bora na wa haki kwa wapiga kura na wagombea kwa ujumla.

Wamesisistiza kuwa rushwa ni adui wa haki, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha hatutoi wala kupokea ili kupata viongozi bora na kudumisha amani iliyopo nchini.

Pia wamewaomba viongozi wa serikali kuwa mabalozi wazuri mitaani na maeneo yao ya kazi kwa kuhakikisha mazingira ya rushwa hayatengenezwi wala kutokea.


No comments:

Post a Comment