Friday, September 06, 2024

*SINGIDA WENYEJI MAONESHO YA (7) YA MIFUKO NA PROGRAMU ZA UWEZESHAJI, WAJIPANGA KUPOKEA WAGENI NA KUHAKIKISHA YANAFANA*

Mkoa wa Singida umejiandaa kikamilifu kuwa wenyeji wa Maonesho ya saba (7) ya kitaifa ya mifuko ya programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi, yatakayofanyika kuanzia Septemba 8 hadi 14, 2024, katika viwanja vya Bombadia.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amesema kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika ili kuhakikisha wageni kutoka mikoa mbalimbali wanapokelewa na kuhudumiwa vizuri huku akisisitiza umuhimu wa wananchi wa Singida kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu.

"Kushiriki katika maonesho haya ni fursa adimu kwa wananchi wetu wa Singida ...tujiandae kupokea wageni wengi na hii kwetu sisi ni fursa kubwa kwa wajasiriamali wetu.....," amesema RC Dendego.

Ameongeza kuwa maonesho haya yanatoa nafasi ya pekee kwa wananchi kupata uelewa wa kina kuhusu programu mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi na jinsi wanavyoweza kunufaika nazo huku akitoa rai kwa wafanyabiashara kutoa huduma nzuri na kuepuka upandishaji wa bei usioeleweka ili wageni watamani kurudi tena Singida.

Akizungumzia hali ya ulinzi na usalama amesema, serikali ya mkoa imejipanga kikamilifu ili kuhakikisha usalama wa wageni na washiriki wote wa maonesho hayo lengo likiwa ni kuboresha nafasi ya Singida kama kituo cha mikutano na maonesho.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bi. Beng’i Issa, ameeleza kuwa maonesho hayo yatakuwa na taasisi nyingi zinazotoa mikopo na ruzuku kwa ajili ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.

"Tuna matarajio makubwa ya watu kushiriki vizuri na kupata huduma na fursa mbalimbali kupitia programu mbalimbali na mifuko ya uwezeshaji hapa nchini. Hii itatusaidia kuinua uchumi wetu binafsi," amesema Bi. Beng’i Issa.

Maonesho hayo yatafunguliwa rasmi na Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, na Uratibu, Mheshimiwa William Lukuvi tarehe 8 Septemba 2024, na kilele chake kitakuwa tarehe 14 Septemba 2024, ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.

No comments:

Post a Comment