Monday, August 12, 2024

TAMISEMI YATOA MAFUNZO YA MPANGO WA SHULE SALAMA KWA WASHIRIKI KUTOKA MIKOA MINNE

Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) leo imeendesha mafunzo maalum ya Mpango wa Shule Salama, yaliyowakutanisha washiriki 275 kutoka mikoa ya Singida, Shinyanga, Tabora, na Simiyu. Mafunzo hayo ya siku tatu yamefanyika mkoani Singida, yakilenga kuwajengea uwezo washiriki ili kuhakikisha shule za sekondari zinatoa elimu bora kwa kuondoa vikwazo mbalimbali vinavyowakabili wanafunzi.

Mafunzo haya yamehusisha wenyeviti wa bodi za shule za sekondari 150, maafisa 12 kutoka ngazi za mikoa, maafisa maendeleo ya jamii ngazi ya mkoa, pamoja na waratibu wa Mpango wa Shule Salama. Aidha, waratibu wa programu ya SEQUIP pia walishiriki katika mafunzo haya, ambayo ni sehemu ya Mpango wa Kuboresha Elimu ya Sekondari wa miaka mitano (2020-2025).

Lengo kuu la mafunzo haya ni kuwapatia stadi na mbinu za usimamizi bora wa shule za sekondari ili kuhakikisha elimu inayotolewa inakidhi viwango vilivyokusudiwa. Mafunzo haya yanazingatia kuondoa vikwazo kama vile ukosefu wa chakula, utoro, na matumizi ya viboko, ambavyo mara nyingi huzuia wanafunzi kufikia malengo yao ya ufaulu. 

Mafunzo haya yanatarajiwa kuwawezesha washiriki kuleta mabadiliko chanya katika shule zao, na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wa sekondari nchini.



Kwa upande wake Afisa Elimu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Elipidus Baganda, akizungumza kwenye mkutano na washiriki wa programu ya Shule Salama amesisitiza umuhimu wa elimu bora kwa wanafunzi kama msingi wa maendeleo ya taifa.

Aidha, alieleza jinsi Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inavyoendelea kutambua na kuthamini elimu kama chombo muhimu cha kuleta maendeleo.

Dkt. Baganda alibainisha kuwa kumekuwepo na changamoto ya mdondoko wa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari, jambo linalozuia wanafunzi kufikia malengo ya kielimu ambapo amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali kupambana na changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu bila malipo na kujenga shule za sekondari karibu na makazi ya jamii, ili kupunguza umbali wa kufuata shule.

Alieleza kuwa Serikali imeanzisha Mpango wa Shule Salama katika shule za sekondari nchini kwa lengo la kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, pamoja na kuongeza ulinzi na usalama wa watoto.

Hata hivyo, Dkt. Baganda amewashukuru wadau wote wanaoshiriki katika kusimamia utekelezaji wa mpango huo na kuwataka washiriki wa mkutano huo kujadiliana na kubadilishana uzoefu ili kuboresha utekelezaji wa mpango wa Shule Salama na kuwataka washiriki kutumia mafunzo hayo kuibua mbinu mpya za kuboresha mazingira ya shule na kuhakikisha wanafunzi wanakamilisha mzunguko wa elimu kwa mafanikio.


Mratibu wa Mafunzo Riaz Abeid, akizungumza kwenye mafunzo ya kuwapatiwa Maafisa na Viongozi stadi za kuweza kusimamia Shule za Sekondari ili ziweze kutoa elimu kwa viwango yanayofanyika Mkoani Singida kwa siku Tatu.

Mafunzo yakiendelea



No comments:

Post a Comment