Monday, September 02, 2024

MAAFISA UGANI SINGIDA WAKABIDHIWA VISHIKWAMBI 206, WATAKIWA KUWA WABUNIFU.

Mkuu wa mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego amewataka Maafisa Ugani mkoani humo kuwa wabunifu katika kuleta mabadiliko kwenye kilimo na utendaji mzuri wa kazi ili kurahisisha ufikiwaji na upatikanaji wa huduma wenye tija kwa wakulima.

Dendego ameyasema hayo leo (Septemba 2, 2024) kwenye hafla ya ugawaji wa vishikwambi 206 kwa Maafisa Ugani wa Halmashauri za mkoani Singida iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.

Aidha, Mkuu wa mkoa amesisitiza utunzaji mzuri wa vishikwambi hivyo ili kuzifanya kudumu kwa muda mrefu na utendaji bora wa kazi huku akiwataka maafisa ugani hao kuhakikisha wanaishi karibu na maeneo yao ya kazi katika kata na vijiji ili kurahisisha ufikiwaji na upatikanaji wao kwa wakati na wananchi wanaohitaji huduma hizo.

Hata hivyo, amewasisitiza uvaaji wa sare za kazi muda wote wawapo kazini ili kutambulika kwa urahisi na wananchi wanaowahudumia katika kata na vijiji vyao na matumizi sahihi ya vifaa walivyopewa ikiwemo vishikwambi, pikipiki na vipimia udongo kama namna ya kuinua kilimo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe.Halima Dendego akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi vishikwambi kwa Maafisa ugani.

"Huwezi kuwekeza kwenye kilimo bila kuwekeza kwenye wataalam, tunataka mkaibadilishe Singida ili wanasingida warudi kwenye kilimo, hakuna namna nyingine ya kumaliza hali duni Singida bila kujituma katika kilimo". alisema RC. Dendego.

Pia, alihimiza maafisa ugani kuhakikisha wanatumia vishikwambi kwa ajili ya kazi pekee na sio shughuli binafsi, akibainisha kuwa vifaa hivyo vimetolewa na serikali ili kuboresha huduma za kilimo na kuinua uchumi wa wakulima. "Ni lazima tuhakikishe tunavitumia kwa lengo lililokusudiwa na kuleta matokeo chanya kwa wakulima na jamii ya Singida kwa ujumla," alisema RC. Dendego.

Katibu Tawala  wa Mkoa wa Singida Dkt.Fatuma Mganga akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi vishikwambi kwa Maafisa ugani.

Naye, Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga, ametoa rai kwa Maafisa ugani wa mkoa huo kutumia vishikwambi walivyokabidhiwa na serikali kwa lengo la kuboresha shughuli za uzalishaji, hususan katika sekta ya kilimo.

Dk. Mganga alisisitiza kuwa vifaa hivyo ni muhimu katika kurahisisha ukusanyaji wa takwimu na ufuatiliaji wa shughuli za kilimo kwa wakulima ili kuongeza tija na ufanisi.

Ameeleza kuwa matumizi sahihi ya vishikwambi hivyo yatawawezesha maafisa ugani kuwa karibu zaidi na wakulima, kutoa elimu ya kilimo, na kutambua changamoto wanazokutana nazo kwa wakati.

Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Natalya Mosha, ameishukuru serikali na kuahidi kuwafikia wakulima wengi kwa muda mfupi baada ya kupata vitendea kazi kama vishikwambi na pikipiki, kutoa maelekezo ambayo wananchi walikua hawawezi kuyapata na wakulima kuongeza uzalishaji katika maeneo yao na hatimaye kuongeza tija katika kilimo.  










No comments:

Post a Comment