Mkuu wa mkoa
wa Singida Halima Dendego amewaagiza Maafisa Afya katika mkoa huo kuwachukulia
hatua kali wananchi ambao watabainika kukaidi kufanya usafi katika maeneo yao
kama hatua ya kuondoa tatizo la magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.
Mkuu wa mkoa
wa Singida ametoa kauli hiyo mara baada ya kumaliza zoezi la kufanya usafi wa
mazingira katika Stendi Kuu ya Mabasi ya Mjini Manyoni.
RC. Dendego amesema mwananchi wa mkoa wa Singida wanao wajibu wa kuhakikisha maeneo yao yanakuwa safi na wanaopuuza sheria za usafi wawajibishwe kwa sababu wanaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo magonjwa ya mlipuko.
“Wananchi tekelezeni
sheria za usafi za Halmashauri na za nchi katika kutunza mazingira yenu ili kuepuka
maradhi yanayozuilika, Amesisitiza Dendego.
Naye, Afisa
Afya wa Wilaya ya Manyoni Seif Swed amesema Halmashauri hiyo imejipanga vizuri
katika zoezi la usafi wa mazingira ambapo wameweka siku ya Jumatano kuwa ni
siku ya usafi kwa wananchi wote na mwisho wa mwezi.
Swed amesema
kwa sasa Halmashauri hiyo ni Moja ya Halmashauri zinazofanya vizuri kwenye
suala la usafi mkoani Singida hivyo amewahimiza wananchi waendelee na moyo huo
katika kufanya usafi ili Halmashauri hiyo iweze kushika namba Moja Kitaifa kwa
usafi wa mazingira.
Baadhi ya
Wananchi wa Wilaya ya Manyoni walioshiriki zoezi la usafi wamesisitiza kuwekwa
mkazo katika matumizi ya sheria hasa kwa wananchi ambao wanakaidi kufanya usafi
kwenye maeneo yao.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego (kulia) akiwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM (MNEC) Mkoa wa Singida Yohana Msita, kwenye zoezi la kufanya usafi wa mazingira katika Stendi Kuu ya Mabasi ya Mjini Manyoni ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya utunzaji wa mazingira.
Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Kemirembe
Lwota (kulia) akishirikiana na moja ya mwananchi kwenye zoezi la kufanya usafi
wa mazingira katika Stendi Kuu ya Mabasi ya Mjini Manyoni ikiwa ni muendelezo
wa kampeni ya utunzaji wa mazingira.
No comments:
Post a Comment