Wednesday, May 29, 2024

KATIBU MKUU WA CCM BALOZI DKT. NCHIMBI AWAPA TANO VIONGOZI WA MKOA WA SINGIDA KWA UTEKELEZAJI BORA YA MIRADI YA MAENDELEO.

Serikali ya mkoa wa Singida imepongezwa kwa kusimamia na kutekeleza kikamilifu Ilani ya Chama ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi kwa kiwango cha juu ikiwemo miradi ya maji, afya, elimu na miundombinu mkoani humo.

Pongezi hiyo zimetolewa na Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi katika ziara yake ya kikazi ya Siku Mbili mkoani Singida wakati anazungumza na wananchi kwenye mikutano ya hadhara katika Wilaya ya Manyoni na Ikungi pamoja na kusikiliza na kutatua papo hapo kero ambazo zilitolewa na wananchi.

Balozi Nchimbi amesema ushirikiano imara kati ya Viongozi wa Serikali na wa CCM mkoani Singida umepelekea miradi mingi ya maendeleo kutekelezwa kwa wakati na kwa kiwango cha juu.

Amesema taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM aliyopatiwa na Mkuu wa mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego, imeonyesha wazi kasi kubwa ya Maendeleo ambayo imepigwa mkoani Singida kwa kuboresha na kuimarisha huduma mbalimbali za Kijamii ikiwemo huduma za maji, afya, elimu,  miundombinu, umeme, pamoja na sekta kilimo kwa usalama wa chakula.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego akitoa salamu za Serikali ya Mkoa huo juu ya utekelezaji wa Ilani kwenye mkutano wa Katibu Mkuu Chama Cha Mapinduzi.

Naye, Mkuu wa mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego, akitoa taarifa ya mkoa wa Singida kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi amemhakikishia Katibu Mkuu huyo wa CCM wataendelea kusimamia kikamilifu fedha ambazo wanapatiwa na Serikali ya awamu ya Sita katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili wananchi waweze kupata huduma bora na za uhakika za maendeleo karibu na maeneo yao.

Halima Dendego amesema mpaka sasa mkoa wa Singida tayari umepokea zaidi ya shilingi Trilioni Moja kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo hali ambayo imeufanya mkoa wa Singida kung’aa kimaendeleo katika sekta mbalimbali.

Mkuu huyo wa mkoa wa Singida amemwomba Katibu Mkuu huyo wa CCM kumfikishia Salamu za pongezi na shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendeleo kuupatia mkoa wa Singida fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.

Amesema mkoa wa Singida kwa sasa unaendelea na mipango na mikakati ya kuwavutia wawekezaji katika sekta mbalimbali wa ndani na nje ya nje kuja kuwekeza mkoani humo ikiwa ni sehemu ya kuongeza pato la mkoa na la taifa kwa ujumla kupitia vivutio vya uwekezaji kwenye masuala mbalimbali ikiwemo kilimo na utalii.




No comments:

Post a Comment