Monday, April 08, 2024

SHEREHE ZA NANENANE KITAIFA MWAKA 2024 KUFANYIKA MKOANI DODOMA, RC DENDEGO AHIMIZA UWAJIBIKAJI

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego, akizungumza wakati wa kikao cha Kamati kuu ya kuratibu Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima (NANENANE) kilichifanyika katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma Aprili 8, 2024

Kamati kuu ya kuratibu Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima maarufu kama Nane Nane kwa Kanda ya kati leo Aprili, 2024 imekutana Jijini Dodoma kwa ajili kupanga mipango mikakati ya kufanikisha maadhimisho hayo yanayotarajiwa kufanika kitaifa kwenye Mkoa wa Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego akizungumza wakati wa kikao hicho amesema kikao hicho kimeonesha dira kwa kuwa wajumbe wamejipanga kikamilifu kuhakikisha maadhimisho hayo yanafana ambapo amewasisitiza kila kamati iliyopangwa ihakikishe inawajibika ipasavyo.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Rosemary Senyamule, akizungumza wakati wa kikao cha Kamati kuu ya kuratibu Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima (NANENANE) kilichifanyika katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma Aprili 8, 2024

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho cha kwanza kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma amewataka washiriki hao kushirikiana kwa pamoja katika maandalizi hayo ya maadhimisho ya Kitaifa kuanzia siku ya kwanza hadi siku ya mwisho.

“Kila mmoja awe sehemu ya maadalizi ili kuhakikisha lengo letu linatimia kwa Kiwango kile tunachotarajia katika sherehe hizi za Kanda ya Kati mwaka 2024" Amesema Mhe. Senyamule.

Kwaupande wake Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Dodoma Bi. Aziza Mumba, amesema kila mwaka (Agosti Mosi hadi 08), Serikali hufanya sherehe za Nane Nane kikanda ikienda sambamba na maonesho mahususi ya wakulima.

"Mkoa wa Singida na Dodoma inayounda Kanda ya Kati, kupitia sherehe hizi ina lengo la kutangaza fursa za uwekezaji, biashara sanjari na kusambaza taarifa za teknolojia na mbinu za Kilimo bora zinazoweza kuwawezesha wakulima kufanya kilimo cha kisasa na kupata mazao stahiki" Bi Mumba.

Kikao hicho kimeazimia mambo kadhaa ikiwemo; kamati ndogo ibainishe na kuongeza taasisi za Wizara ya Kilimo na Misitu, Taasisi za Misitu zihusishwe ipasavyo kwani Sekta ya Kilimo inahusisha Mazao, Mifugo, Uvuvi, Madini na Misitu, kuweka Kongamano la siku moja la Uwekezaji litakaloangazia fursa za Sekta zote, Kamati ziundwe na kuridhiwa mapema, Uwepo wa Utalii wa kutembelea miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa, Mpango kazi uwe na muda wa utekelezaji.

Baadhi ya Wajumbe kutoka Serikali ya Mkoa wa Singida wa Kamati kuu ya kuratibu Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima (NANENANE) yanayotarajiwa kufanyika Kitaifa Jijini Dodoma mwaka huu wakifuatilia jambo wakati wa kikao hicho kilichifanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma Aprili 8, 2024
Kutoka kushoto ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Thomas Apson na Mkuu wa Wilaya ya Singida Godwin Gondwe.

Baadhi ya Wajumbe kutoka Serikali ya Mkoa wa Dodoma wa Kamati kuu ya kuratibu Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima (NANENANE) yanayotarajiwa kufanyika Kitaifa Jijini Dodoma mwaka huu wakati wa kikao hicho kilichifanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma Aprili 8, 2024

Kikao kikiendelea

No comments:

Post a Comment