Monday, April 08, 2024

RC SINGIDA ATOA SIKU 30 KWA MKURUGENZI MANYONI KUPIMA NA KUWEKA ALAMA KITUO CHA WAZEE WASIOJIWEZA CHA SUKAMAHELA.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego, (wa pili kutoka kulia), Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Singida Mheshimiwa Martha Mlata (wa kwanza kushoto), Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga (wa kwanza kulia) wakikabidhi moja ya zawadi kwa wazee wasiojiweza katika kituo cha Sukamahela Wilayani Manyoni.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego, ametoa muda wa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kutuma timu ya Wataalamu wa Ardhi kwenda katika Kituo cha Makazi ya Wazee wasiojiweza cha SUKAMAHELA kwa ajili ya kupima na kuweka mipaka ya kituo hicho ili kudhibiti wananchi wasivamie eneo hilo na kuanzisha shughuli za kiuchumi ikiwemo mashamba.

Dendego ametoa kauli hiyo leo (8-Aprili-2024) baada ya kutembelea Kituo hicho na kukabidhi zawadi mbalimbali kutoka kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo Televisheni, friji, nguo, vyakula kwa ajili ya sikukuu ya EID.

Aidha, amesisistiza kuwa baada ya mwezi mmoja kuisha apatiwe taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo vinginevyo atawachukulia hatua Watendaji ambao hawatatekeleza agizo hilo nia ikiwa ni kuhakikisha Wazee wanaotunzwa kwenye kituo hicho wanakaa na kuhudumiwa vizuri bila ya kubughuziwa na mtu.

“Hawa Wazee wametutumikia sana wametufanya tuwe hapa tulipo hivyo ni lazima tuwaheshimu, tuwalee na Tuwatunze” Alisisitiza DENGEGO.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego, akisisiza jambo kwa Watendaji wa Mkoa huo kutenga muda kuwatembelea wazee wenye uhitaji ili kuwatia moyo na kuwapa faraja.

Kuhusu tatizo la kukosekana kwa huduma ya maji na umeme kwenye kituo hicho ambacho kilianzishwa mwaka 1974 kwa ajili ya kutoa huduma kwa Waathirika kwa ukoma, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka Watendaji wa Shirika la Ugavi wa Umeme - TANESCO – Mkoani Singida na wa Mamlaka ya Maji waende kwenye kituo hicho na kuweka kambi ili huduma hizo muhimu ziweze kupatikana muda wote kwenye kituo hicho.

Amefafanua kuwa siku 14 zinatosha kabisa kuweka huduma za maji na umeme kwenye kituo hicho kama hatua ya kuhakikisha wazee hao wanaishi maisha yenye staha ikilinganishwa na hali ilivyo kwa sasa.

Amesisitiza kuwa kupatikana kwa huduma hizo kutasaidia ulinzi kwa wazee hao pamoja na kuwaepusha na vitendo vya kushambuliwa na wanyama wakali hasa nyakati za usiku.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga, akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi zawadi kwa wazee wasiojiweza katika kituo cha Sukamahela Wilayani Manyoni.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga, amesisitiza Watumishi wa Serikali wanaofanya kazi kwenye kituo hicho kufanya kazi kwa weledi, bidii na ufanisi katika kuwalinda na kuwatunza Wazee hao ili waishi maisha mazuri na yenye furaha kama watu wengine.

Amesema kuwa Wazee ni hazina na baraka hivyo lazima wahudumiwe ipasavyo na kupatia huduma za msingi kama jamii nyingine.

Mkuu wa Kituo cha Makazi ya Wazee wasiojiweza cha Sukamahela Bi. Kusajo Kafuko, ametaja changamoto mbalimbali zinazokwamisha utoaji wa huduma bora kwa wazee hao ikiwemo kukosekana kwa huduma maji, umeme pamoja na kukosekana kwa mlezi wa kiume.

Ameeleza kuwa anaimani kubwa kuwa ujio wa viongozi hao utasaidia kutatua changamoto hizo ambazo zinakwamisha utoaji wa huduma bora kwa Wazee hao walemavu.

Kituo cha Makazi ya Wazee Wasiojiweza cha SUKAMAHELA wilayani MANYONI kilianzishwa mwaka 1974 kwa ajili ya kutoa huduma za tiba kwa Waathirika wa ugonjwa wa ukoma ambapo kwa sasa kinahudumia wazee kutoka Mikoa ya SINGIDA na DODOMA.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Singida Mheshimiwa Martha Mlata akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa huo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi zawadi mbalimbali kwa wazee wasiojiweza katika kituo cha Sukamahela Wilayani Manyoni.


Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (MNEC) Mkoa wa Singida, Yohana Msita, akizungumza kwenye hafla hiyo.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Singida Lucy Boniphace, akizungumza kabla ya kumkaribisha Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa huo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi zawadi mbalimbali kwa wazee wasiojiweza katika kituo cha Sukamahela Wilayani Manyoni.


No comments:

Post a Comment