MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, ametoa muda wa mwezi moja
kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa huo kumpatia taarifa za vifaa tiba
vilivyoletwa na Serikali kwenye Hospitali za Wilaya, Zahanati na Vituo vya Afya
ili kuweka mkakati wa kutunza vifaa hivyo ipasavyo.
Dendego ametoa kauli hiyo leo Machi 27, 2024 Wilayani Ikungi katika
mwendelezo wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo pamoja na
kuzungumza na Viongozi, Watumishi wa Umma, na Wakuu wa Taasisi za Umma mkoani
humo.
Amesema vifaa vinavyotolewa na Serikali katika Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati nchini ni ghali mno hivyo ni muhimu kwa kila watumishi kuhakikisha wanavitumia kwa ufasaha katika kutoa huduma bora kwa wananchi na kuvitunza ili viweze kudumu kwa muda mrefu.
“Haya majengo ni yetu sote wala hayajamlenga mtu yeyote ni
sisi tuliokuwepo hapa na wengine ni muhimu yakalindwa na kutunzwa kwa sababu
huwezi kujua siku wala saa utakapoumwa”
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego akizungumza na Watumishi wa Umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida
Kuhusu huduma za Wazee, Mkuu wa Mkoa huyo ameagiza kila
Halmashauri katika Mkoa huo kutenga bajeti kwa ajili ya kununulia dawa za Wazee
kama hatua ya kuondoa malalamiko kuhusu uduni wa utoaji wa huduma za afya katika
kundi hilo.
Amesisitiza kuwa itakuwa ni jambo zuri kama hata maeneo yanayotoa
huduma za matibabu kwa wazee yawekewe maji na chai kwa sababu Wazee hao
wametumikia Taifa hivyo ni muhimu wakatunzwa na kuhudumia vizuri.
“Tengeni fedha zinazotokana na mapato ya ndani kwa ajili ya
kununua dawa za wazee kwa sababu magonjwa yao yanajulikana” Dendego amesisitiza.
Nao Viongozi wa Wilaya ya Ikungi wamemshukuru Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa upatikanaji wa fedha za kutusho hususan ndani ya uongozi wake
wa miaka mitatu kuwezesha ukamilishaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na
kumuahidi Mkuu huyo wa Mkoa kutekeleza maagizo aliyoyatoa ili wananchi waweze
kupata huduma bora na za uhakika karibu na maeneo yao.
Akiwa Wilayani Ikungi, Dendego ametembelea na kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo mradi wa maji wa kijiji cha Matare, Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Ujenzi wa barabara ya Matongo kwa kiwango cha lami na Shule ya kisasa ya Mtaturu.
MATUKIO KATIKA PICHA
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego akizungumza na Wanafunzi wa shule ya Msingi Mtaturu iliyopo Wilayani Ikungi wakati wa ziara yake.
No comments:
Post a Comment