Tuesday, March 26, 2024

RC DENDEGO AZIAGIZA HALMASHAURI MKOANI SINGIDA KUWASIMAMIA WAKANDARASI IPASAVYO

MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, ameagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA) kuhakikisha wanasimamia kwa karibu mradi wa ujenzi wa mabwawa ya kutibu majitaka unaojengwa katika Manispaa ya Singida kwa Sh.bilioni 1.7 ili ujengwe vizuri ulingane na thamani ya fedha.

Ametoa agizo hilo leo (tarehe 26 Machi, 2024) baada ya kufanya ziara ya kutembelea mradi huo ambao unajengwa eneo la Manga ambapo alisema Serikali imetoa fedha nyingi kutekeleza mradi huo hivyo haitegemei baada ya muda mfupi uharibike kutokana na kutojengwa vizuri.

"Meneja wa SUWASA mbane mkandarasi ahakikishe anajenga mradi vizuri ili thamani ya fedha ionekane hatutegemei mradi ukae muda mfupi uanze kuharibika, nawapongeza Manispaa kwa kupata mradi kama huu,"alisema.

Awali akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Meneja wa SUWASA, Sebastian Warioba, alisema mradi huo umeanza kujengwa Mei mwaka jana na unatarajia kukamilika Novemba mwaka huu na hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 46 na mabwawa mawili yamekamilika.

Meneja wa Mamlaka ya Majisa na Usafi wa Manzingira Mkoa Singida (SUWASA) Sebastian Warioba, akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Halima Dendengo (kushoto), wakati wa ziara yake katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida Machi 26, 2024.

Warioba alisema kujengwa kwa mradi huu ni ukombozi mkubwa kwa Manispaa ya Singida kwani kwa kipindi kirefu majitaka yalikuwa yakitupwa porini jambo ambalo kiafya sio zuri.

"Faida ya mradi huu kwa wananchi utawawezesha kupata huduma ya usafi wa mazingira kwa kuondoa majitaka kwenye makazi yao na kuongeza shughuli za maendeleo ikiwemo kuendesha kilimo cha mboga mboga," alisema.

Warioba alisema Singida imebahatika kuwekwa katika mpango wa mradi wa miji kumi ambao utawezesha kujengwa kwa mtandao wa majitaka kwa kujengwa kutoka kwenye majumba.

Mkuu wa Mkoa akiwa katika mradi wa kituo cha Afya Mtipa, aliipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Singida kwa kujenga kituo hicho kutumia fedha za makusanyo ya ndani zaidi ya Sh.milioni 500.

Mkuu wa Mkoa Singida Mhe. Halima Dendego, (wapili kutoka kushoto) akiwa katika mradi wa kituo cha Afya Mtipa Halmashauri ya Manispaa ya Singida wakati ziara ya ukaguzi wa miradi. (kushoto kwake) ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Godwin Gondwe.

Dendego alisema yeye pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe kituo hicho kitakapokamilika watapambana kuhakikisha vifaa tiba vinapatikana ili huduma za matibabu zianze kutolewa haraka.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Jeshi Lupembe, alisema kituo hicho cha afya kilianza kujengwa Februari 2023 kinatarajia kukamili Mei mwaka huu na kitatoa huduma kwa wananchi wa kata ya Mtipa na kata jirani.

Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa alitembelea Kituo cha Afya Mtipa, Mabwawa ya kutibu majitaka, ujenzi wa nyumba ya mwalimu na ujenzi wa zahanati ya Ititi.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego (kulia) akipokea taarifa ya mradi wa ujenzi wa nyumba ya Mwalimu katika shule ya Sekondari Uhamaka iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Singida Machi 26, 2024.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego (kushoto) akitoa maelekezo kwa viongozi wa Halmashauri ya Manispaa katika Kituo cha Afya Mtipa kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Singida Machi 26, 2024.

Moja ya sehemu ya jengo la Kituo cha Afya Mtipa.



Jengo la Utawala katika shule ya Sekondari Uhamaka

Mkuu wa Mkoa wa Singida akiwa katika picha ya pamoja wakati alipotembelea Zahanati ya Ititi Halmashauri ya Manispaa. Kulia na kushoto kwake ni baadhi ya wananchi waliofika kupata huduma za matibabu.

No comments:

Post a Comment