Tuesday, March 12, 2024

RC DENDEGO APOKELEWA KWA KISHINDO MKOANI SINGIDA NA KUKADHIWA RASMI OFISI

Mkuu mpya wa Mkoa wa Singida Halima Dendego, ameahidi kusimamia shughuli za maendeleo kwa niaba ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, na kutoa tahadhari kwamba kwenye uongozi wake hataki kusikia suala la msamiati wa changamoto kama sababu mojawapo ya kukwamisha maendeleo.

Dendego amesema hayo muda mfupi alipokabidhiwa ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Peter Serukamba, na kuzungumza na Watumishi wa ofisi hiyo, Kamati ya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa vyama vya siasa, Viongozi wa Dini na wageni waalikwa mbalimbali.

"Nimekuja Singida kupokea majukumu ya kazi niliyopewa na Mheshimiwa Rais wa Hamguri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, kama alivyoacha kaka yangu Serukamba, na mimi nitasimamia ili tupige hatua mbele zaidi, nawahakikiahi kama aliyeondoka ni Kulwa, basi aliyekuja ni Doto...lazima kazi ziendelee kwa ajili ya kuleta maendeleo." alisema Dendego.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego (kushoto) akipokelewa na vijana wa skauti mara baada ya kuwasili katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida kwaajili ya makabidhiano na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Peter Serukamba(hayupo pichani).

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amesema ni lazima kazi zifanyike na majibu yapatikane katika utumishi wake huku akaisisitiza kuwa atakuwa msikivu mnyenyekevu na mtulivu kwa anaowaongoza na kusimamia shughuli na miradi ya maendeleo mkoani Singida.

Amewahakikishia utumishi uliotukuka na ushirikiano wa dhati watumishi wote wa Mkoa wakiwemo wakuu wa Wilaya za Mkoa, Wakurugenzi wa Halmashauri ili kuwaletea maendeleo ya dhati wananchi na Watanzania kwa ujumla wa Mkoa wa Singida.

Akizungumza kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Singida, Katibu Mwenezi wa chama hicho pamoja na kuwapongeza wakuu hao wa mikoa, alisema CCM itaendeleza ushirikiano wa dhati na Serikali ya Mkoa kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba, akizungumza na viongozi na baadhi ya wananchi walioshiriki katika hafla ya makabidhiano ya ofisi yalifofanyika leo Machi 12, 2024 mkoani Singida.

Awali aliyekuwa Mkuu wa Mkoa aliyehamishiwa mkoani Iringa, Peter Serukamba, alitumia fursa hiyo kuzishukuru kada mbalimbali za uongozi tangu awasili mkoani Singida mwaka mmoja na miezi saba iliyopita na kufafanua kuwa amejifunza mengi ya maendeleo akiwa Singida.

Serukamba alisema akiwa Singida anajivunia kupandisha matumizi ya mbolea ikilinganishwa na hali aliyoikuta huku pia akifanikisha upatikanaji wa mbegu ya ruzuku kwa zao la alizeti.

Serukamba alisema pia katika kipindi chake mkoani Singida anajivunia kumaliza tatizo la mauaji lililokuwa linaikabili Wilaya ya Manyoni kutokana na kukithiri kwa mauaji nyakati za usiku na ufukuaji wa makaburi kutokana na imani za kishirikina.

Amesema kwa nguvu hiyo hiyo, ndiyo atakayoenda nayo Iringa, kwa lengo la kupambana na kuongeza juhudi ili asiyashushe maendeleo ya mkoa huo yaliyochagizwa na Mkuu wa Mkoa Halima Dendego, aliyehamishiwa sasa mkoani Singida.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Singida, Katibu mwenezi wa CCM, Elphas Lwanji amesema kuwa, chama hicho kinaahidi kushirikiana na Serikali ya Mkoa huo kupitia uongozi wa Halima Dendego, kama ambavyo walimpatia Peter Serukamba.

Mkuu mpya wa Mkoa wa Singida Halima Dendegoakizungumza na viongozi na baadhi ya wananchi walioshiriki katika hafla ya makabidhiano ya ofisi yalifofanyika leo Machi 12, 2024 mkoani Singida.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba, akimkabidhi taarifa ya Mkoa wa Singida kwa Mkuu wa Mkoa huo Halima Dendego, wakati wa hafla ya makabidhiano ya ofisi.

Wakuu wa Mikoa wakiweka saini katika vitabu vya makabidhiano ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa Singida Machi 12, 2024























No comments:

Post a Comment