Monday, December 04, 2023

SUALA LA VIJANA KUJIKITA KWENYE KILIMO SIO HIARI BALI NI LAZIMA - RC PETER SERUKAMBA:

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba ameagiza Watendaji wa Kata, Vijiji na Mafisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, kuwahamasisha wananchi hususani vijana wajikite kwenye kilimo cha mazao ya biashara na chakula ili kuongeza uzalishaji hasa zao la Alizeti kutoka asilimia 50, msimu uliopita hadi kufikia 70, msimu huu (2023/24).

Serukamba amesema hayo leo Desemba 4, 2023 kwenye kikao chake na Watendaji wa Kata, Vijiji na Maafisa Ugani, katika kikao kilichofanyika ukumbi wa Halmashauri hiyo lengo likiwa ni kujadili hatima ya kilimo ili kuongeza maeneo ya kilimo kwa ajili ya msimu huu 2023/2024.

“Ndugu zangu, hapa sitanii, nataka tujiandae kusimamia kilimo, suala la watu kwenda shambani ni la lazima sio hiari, watu wote waende wakalime, tukifanya hivyo tutapata mavuno yatakayoondoa changamoto ya umasikini kwa watu wetu…tunataka Mkoa wa Singida uingie kwenye historia ya kuzalisha mafuta ya alizeti ili Taifa litutegemee kwa mafuta ya kula,” alisema Serukamba.

Kuhusu msimu uliopita, Mkuu huyo wa Mkoa amesema, alizeti iliyozalishwa nchini Mkoa wa Singida ulichangia asilimia 50, akasisitiza kuwa msimu huu anataka kuona Mkoa unapiga hatua zaidi hadi kufikia asilimia 70, na kiwango hicho kitafikiwa iwapo wakulima wataongeza nguvu katika kilimo kwa kushirikiana na wataalamu wa Ugani, Watendaji wa Vijiji na Kata.

Juu ya suala la mbegu bora, Serukamba amewaeleza wadau hao kuwa Serikali imekubali kuupatia Mkoa wa Singida mbegu mpya aina ya Haysan, itakayouzwa kwa bei ya ruzuku kwa ajili ya kutoa nafuu kwa mkulima kuweza kuzalisha kwa wingi zao la Alizeti.

Pia Mkuu huyo wa Mkoa alisistiza umuhimu wa matumizi ya mbolea kwa ajili ya kuleta tija na kuongeza uzalishaji wa mbegu za Alizeti shambani hivyo kumaliza kabisa tatizo la mafuta ya kula hapa nchini.

“Hatuwezi kuongeza mazao au kuleta tija kama hatutumii mbolea, naomba sana ndugu zangu tuwasimamie wakulima wetu watumie mbolea kwa wingi ili wanufaike na kazi ya kilimo, tukifanya hivi Halmashauri nayo itafaidika kwa kupata mapato mengi yatakayotumika kwa kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo,”alisistiza Serukamba.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa, amesema Serikali ya Mkoa wa Singida imeanzisha mfumo mpya wa stakabadhi ghalani itakayohusisha mazao mbalimbali yakiwemo dengu, choroko alizeti na korosho, kuanzia msimu ujao ambayo yatauzwa kwa mfumo huo ili wakulima waweze kunufaika zaidi na hivyo kukuza uchumi wao.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili, alimhakikishia Serukamba kuwa maeneo yaliyoainishwa kupitia kikao hicho yanayofikia zaidi ya ekari 702, yote yatalimwa kutunzwa na kuhakikisha wakulima wanatumia mbegu bora na mbolea ili kuongeza tija katika uzalishaji hoja iliyoungwa mkono na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson wakati Mkuu huyo wa Mkoa alipokuta na Watendaji wa Kata, Vijiji na Maafisa Ugani pamoja na Watumishi wa Halmashauri hiyo ya Ikungi Desemba 4, 2023.

Katika kikao kazi hicho walikubaliana kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Singida itaongeza eneo la kilimo msimu huu linalofikia ekari 702, huku Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ikiazimia kuongeza eneo la kilimo ekari 2,200, katika msimu huu wa kilimo 2023/2024.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, akizungumza na  Watendaji wa Kata, Vijiji na Mafisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida wakati wa kikao hicho.

Watendaji wa Kata, Vijiji na Mafisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida wakati wa kikao hicho kikiendelea.

Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Muragili, akuzungumza wakati wa kikao hicho.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Thomas Apson, akizungumza wakati wa kikao hicho.

No comments:

Post a Comment