Friday, December 01, 2023

WATENDAJI KATA, VIJIJI NA MAAFISA UGANI, SIMAMIENI KILIMO BORA - RC SERUKAMBA

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, amewataka Watendaji wa Kata, Vijiji na Maafisa Ugani wawaelekeze Wakulima umuhimu wa kanuni na taratibu za Kilimo bora ili waongeze uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kwa lengo la kuwakwamua kiuchumi wananchi wa Singida na Taifa kwa ujumla.

Serukamba ametoa maelekezo hayo leo Ijumaa Disemba Mosi, alipokutana nao kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, pamoja na mambo mengine kuandaa kwa pamoja mikakati ya kilimo itakayoongeza eneo la Kilimo, kupitia mazao ya chakula na biashara mkoani Singida.

“Nataka niwaambieni, kwenye hili hatutanii Watendaji wa Kata!, naomba niwaambieni, hili jambo kwangu ni la kufa na kupona…mkitoka hapa, muende mkakutane na Serikali za kijiji, mkafanye mikutano, hakikisheni tunalima eneo jipya, ambalo mwaka jana halikulimwa, mkahakikishe vijana wote wanaozurura bila kazi kwenye maeneo yenu wanashiriki katika kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara…,” alisisitiza Serukamba.

Aidha Serukamba, ameeleza kuwa Serikali imekubali ombi la Wakulima la kupatiwa aina mpya ya mbegu ya zao la Alizeti badala ya ile ya msimu uliopita ili waongeze uzalishaji wa mafuta ya kula nchini ambayo kwa msimu uliopita Mkoa wa Singida ulichangia zaidi ya asilimia 50 ya alizeti yote inayozalishwa hapa nchini.

Katika makubaliano ya Watendaji hao wa Wilayani Mkalama na Mkuu wa Mkoa iliazimiwa kwamba eneo la kilimo msimu huu wa 2023/2024, liongezwe ekari 9,940 zaidi ili kuongeza wingi wa mazao ya chakula na biashara wakati msimu wa 2022/2023 Wilaya ya Mkalama ililima eneo lenye ukubwa wa ekari 354,230.

Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Sekretarieti ya Mkoa Singida Stanslaus Choaji, amewataka Watendaji hao wa Kata na Vijiji, wakasimamie zoezi hilo sambamba na kurejesha fedha za ruzuku ya mbegu ya Alizeti waliyokopeshwa wakulima msimu uliopita, lakini baadhi yao wamegoma kurejesha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mashaka juu ya ubora wake.

“Kimsingi ni majukumu yetu hapa sote, Watendaji wa Kata na Vijiji kufanikisha suala hili kwa hiyo tunampongeza sana Mkuu wetu wa Mkoa kutukumbusha leo, na naamini kutokana na Kikao hichi sasa tunakwenda kusimamia vyema zoezi hili ili Wakulima wetu waweze kunyanyuka zaidi Kiuchumi,” alisema Choaji.

Hata hivyo kwa kuonyesha kwamba maagizo ya Serukamba yamewaingia vyema, Mtendaji wa Kata ya Mwanga, Hamisi Soya, aliwasimamisha Watendaji wa Vijiji vya Kata yake mbele ya Mkuu wa Mkoa na kuwataka hadi kufikia siku ya Jumatatu Novemba 4, 2023, wawe wameitisha mikutano ya hadhara ili kwa makubaliano na Wananchi waongeze ekari 700, kukidhi matakwa ya Serikali ya Mkoa.

“Mimi kwenye Kata yangu ya Mwanga, ninao uwezo wa kuongeza ekari 700, nitazitoa wapi!, Watendaji wa Vijiji vyangu naomba msimame wote, nawaagiza Jumatatu mfanye mikutano mtoe tatizo hili la vijana kuzurula badala kufanya kazi, walazimisheni waende kutafuta mashamba kila mmoja angalau alime ekari mbili, kama tulivyokubaliana. Naomba mkae…kwa hiyo Mkuu wa Mkoa hii siyo lelemama, tunaenda kupambana kweli kweli, na tunahakukikishia zoezi hili litakamilika, kwa asilimia mia,” alimaliza Soya.

Kutokana na Kata ya Mwanga kuwa na eneo pana kwa ajili ya shughuli za kilimo, hata hivyo wajumbe wa Kikao hicho walikubaliana Kata hiyo iongezewe eneo la kilimo hadi kufikia ekari 2,000, badala ya 700, na Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwanga (Soya), alikubali na kuahidi kutekeleza msimu huu wa kilimo 2023/2024.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akisisitiza jambo kwa Watendaji wa Kata, Vijiji na Maafisa Ugani wakati wa kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Moses Machali akizungumza na Watendaji wa Kata, Vijiji na Maafisa Ugani wakati wa kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama



Baadhi ya Watendaji wa Kata, Vijiji na Maafisa Ugani wakimuahidi Mkuu wa Mkoa huyo utekelezaji wa maazimio ya kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama


Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Sekretarieti ya Mkoa Beatus Choaji, akizungumza katika kikao hicho.


Kikao kikiendelea

No comments:

Post a Comment