Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa
Uhuru Kitaifa mwaka 2023, Abdalla Shaib Kaim amesema kuwa miradi ya maendeleo
iliyokaguliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu katika Halmashauri ya
Manispaa ya Singida imetekelezwa kwa viwango vinavyokubalika na kutekelezwa
kizalendo.
Kaim ametoa kauli hiyo leo
tarehe 25 Septemba, 2023 wakati wa ziara ya ukaguzi, uzinduzi na uwekaji wa
jiwe la msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida.
Kaim akiweka jiwe la msingi
katika Kituo cha Afya Mtipa, amesema kuwa miradi mingi imetekelezwa kwa viwango
vinavyokubalika na kuzingatia ubora na thamani ya fedha.
Akizungumzia mradi wa Kituo
cha afya cha Mtipa, Kaim amesema kuwa mradi huo umejengwa kwa kiwango na ubora
sambamba na uwepo umakini katika nyaraka mbalimbalimbali za manunuzi na
utekelezaji wa mradi.
Hata hivyo amewataka
Wakandarasi wanaofanikiwa kupata tenda za kujenga miradi mbalimbali ya Serikali
wanatakiwa kuwa wazalendo kwa kuhakikisha wanajenga miradi hiyo kwa viwango
ubora unaokubaliwa na Serikali.
Aidha amewataka wakandarasi
kuhakikisha wanamaliza miradi yao kwa wakati ili iweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa
na si vinginevyo.
Katika hatua nyingine Kiongozi
wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 ametembelea na kukagua mradi wa
uboreshaji wa huduma wa usafi wa mazingira katika Manispaa ya Singida.
Sambamba na hilo amewataka
wananchi wa Singida Mjini kuhakikisha wanatunza mazingira kwa kupanda miti na
kuitunza. Aidha amewataka wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha changamoto zote zilizotolewa maelekezo yanafanyiwa kazi kwa wakati.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya
ya Singida Mhandisi Paskas Muragili amesema miradi iliyozinduliwa na Mbio za
Mwenge wa Uhuru mwaka huu pamoja na kukaguliwa na kuwekwa jiwe la msingi
itatunzwa na kulindwa na ile ambayo haijakamilika itakamilishwa kwa wakati.
Sambamba na hilo Mhandisi
Muragili, amesema miradi inayotekelezwa inalenga kuwanufaisha wananchi na
kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali zinatumiwa kwa malengo
yaliyokubalika.
Jumla ya sh. Bilioni 3.113
zimetumika kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya
Manispaa ya Singida. Katika ujenzi wa miradi hiyo imewashirikisha wananchi,
wadau (wahisani) pesa za ndani kwa maana ya vyanzo vya mapato kutoka
Halmashauri ya Manispaa ya Singida na fedha kutoka Serikali Kuu.
Kwenye utekelezaji wa miradi
hiyo wanachi wamechangia kiasi cha fedha Milioni moja, wahisani Bilioni 1.7,
Manispaa shilingi Milioni 511 na Serikali Kuu imechangia kiasi cha Shilingi
Milioni 870.4 na kufanya jumla ya sh Bilioni 3.113
No comments:
Post a Comment