Wasimamizi wa Miradi ya maendeleo mkoani Singida wametakiwa kuweka kumbukumbu sahihi ya miradi hiyo kila hatua inayofikiwa (documentation) jambo ambalo litawasaidia katika utoaji wa taarifa kwa viongozi mbalimbali pindi watembelewapo kwenye miradi hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, wakati wa makabidhiano baina ya Katibu Tawala Mstaafu Dorothy Mwaluko na Katibu Tawala mpya Dkt. Fatma Mganga katika hafla iliyofanyika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkoa huo.
Serukamba amesema kwamba wasimamizi wengi wa miradi wanapata wakati mgumu kuielezea miradi wanayo isimamia kwa sababu wanakuwa hawana kumbukumbu za kutosha kuhusu miradi yao.
Aidha amesema kwa kuacha kuweka kumbukumbu sawa za miradi kunasabisha watumishi kutoa taarifa zisizo za ukweli jambo ambalo limekuwa likiwasumbua viongozi mbalimbali kwa kupatiwa taarifa zisizokuwa sahihi.
"Kila kitu unachokifanya kwenye mradi hakikisha unaweka kumbukumbu kwenye faili hii itasaidia baadhi ya watumishi wa Halmashauri kusema habari zilizokuwa za ukweli, " alisema RC Serukamba.
"Niwakumbushe kwamba RAS mpya alishakuwa Mkurugenzi kwenye Halmashauri hivyo hamtaweza kudanganya" Aliendelea kueleza.
Hata hivyo amemshukuru RAS Mwaluko kwa jitihada zake za kufanikisha miradi mbalimbali mkoani hapo huku akiahidi ushirikiano mkubwa kwa Katibu Tawala mpya aliyekabidhiwa Ofisi.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga amewataka watumishi kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufikia malengo huku akiwakumbusha kwamba katika kipindi chake hatahitaji majungu kwakuwa hayana mchango wowote katika kuwanufaisha wananchi wa Mkoa huo.
Awali Viongozi wa dini walipokuwa wakifanya maombi waliwasihi watumishi kufanya kazi kwa uadilifu na kuziheshimu nyazifa walizonazo ili waweze kuwasaidia Wananchi wa Mkoa huo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment