Wednesday, March 22, 2023

Manyoni watakiwa kupima viwanja ili kufidia madeni.

Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida imeelekezwa kutafuta eneo na kupima viwanja ili vigawiwe kwa wananchi ambao wanaidai Halmashauri hiyo na watakao kataa waendelee kusubiri fedha za fidia.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba baada ya kusomewa  taarifa na kamati aliyokuwa ameichagua ikiwa na lengo la kushughulikia migogoro kumi (10) ya ardhi, kamati ambayo imebainisha kwamba wapo wananchi ambao wanatakiwa kulipwa fidia ya viwanja vilivyochukuliwa na Halmashauri hiyo.

RC Serukamba amesema Halmashauri hiyo ishirikiane na Mwenyekiti wa Halmashauri Jumanne Mlagaza  pamoja na Madiwani wote ili kupata eneo hilo  ambapo watatakiwa kuhakikisha miundombinu muhimu inafikishwa katika eneo hilo.

Aidha amesema atawasiliana na Shirika la ugavi wa Umeme  TANESCO, Wakala wa Barabara za mijini na Vijijini TARURA  na  Wakala wa Usambazaji maji na usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA ili kutafuta namna ya kupeleka miundombinu hiyo katika eneo litakalochaguliwa na Halmashauri hiyo.

Hata hivyo Serukumba amefafanua kwamba viwanja hivyo vitagawiwa kwa walengwa kulingana na madai yake na haitakuwa lazima ila kwa mtu atakekubali huku akibainisha kwamba atakaye kataa atapewa fedha zake za fidia kama ilivyokubalika.

Awali akitoa taarifa ya kamati Kamishina wa ardhi Mkoani hapo Shamimu Hoza amesema migogoro mingi ya ardhi Wilayani hapo inasababishwa na taasisi zinazohusika kutowasiliana katika umilikishaji wa ardhi na upangaji wa vijiji ambapo vingine vimekuwa ndani ya hifadhi jambo ambalo linasababisha kutokea kwa migogoro.

Aidha ametoa angalizo kwa wananchi hao kwamba kufyeka pori hakutoi umiliki wa eneo hivyo kila mwenye uhitaji wa ardhi anapaswa kufuata njia zinazostahili ili kupata eneo.

Kamati hiyo ilikuwa ikichunguza migogoro kumi 10 ya ardhi kwenye eneo la viwanja mashamba na mauaji ya wananchi yenye sura ya kishirikiana na imani potofu.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akisisitiza jambo wakati wa mkutano huo.

Kamishina wa Ardhi Mkoa wa Singida Shamimu Hoza, akizungumza wakati wa mkutano huo.

Mkutano ukiendelea

No comments:

Post a Comment