Saturday, March 11, 2023

TUJIRIDHISHE NA UWEPO WA VIKUNDI VYA VIJANA KABLA YA KUWAKOPESHA

 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amezitaka Halmaashuri za Mkoa huo kutoa mikopo ya vijana na wanawake baada ya kujiridhisha na uwepo wa kikundi na shughuli zinazofanywa na kikundi husika.

Amesema hafurahishwi na vitendo vya vikundi vinavyoundwa baada ya kupata pesa wakishagawana wanapotea na Halmashauri zinashindwa kuwadai huku wengine kutumia fedha za mkopo kujenga na wengine kuolea bila kujua fedha hizo zinatakiwa kurudi Serikalini.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya  Mkoa ilipokutana katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi hizo ambapo taarifa zilionesha vikundi vingi katika Halmashauri mbalimbali hukopesha lakini hakuna mradi wa maana ulianzishwa.

" Wapo watu wanajiunga watano hawana wazo la mradi mnawapa fedha wanagawana baadae mnashindwa kuwadai na fedha zinapotea, tutumie fedha hizo kuwaendeleza watu na sio kuwafurahisha " Alisema Serukamba.

Aidha amewataka Wakurugenzi kabla hawajatoa mikopo hiyo kwa vijana na wanawake kujiridhisha kwa kuona mipango ya mradi na kuwashauri ili miradi iweze kusimama na kuhakikisha fedha inayotolewa inafanya kilichokusudiwa.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Mwl. Dorothy Mwaluko akizungumza wakati wa kikao hicho.

Hata hivyo RC Serukamba ametumia muda huo kuwapongeza Halmashauri ya Ikungi ambavyo vikundi vilivyoanzishwa vimeendelea vizuri na vinajiongezea kipato.

"Hakikisheni mnatembelea vikundi mjue kazi wanazozifanya kabla hajawakopeshwa, na tumieni muda huo kuwafundisha wenye nia ya kuanzisha mradi." Alieleza

Mikopo hiyo inalenga asilimia nne kwa vijana asilimia nne kwa wanawake na asilimia nne kwa wenye ulemavu ambapo kila Halmashauri inatakiwa kutumia fedha za ndani kuwakopesha wahusika.




No comments:

Post a Comment