MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter
Serukamba, ametoa siku saba kwa watumishi wa Idara ya fedha ya Halmashauri ya Wilaya
ya Iramba kuzirejesha Sh.Milioni 365 ambazo ni fedha zilizokusanywa na watumishi
na mawakala kama ushuru na kodi kutoka kwa wananchi.
Watumishi na mawakala hao
walizikusanya fedha hizo badala ya kuzipeleka benki kwenye akaunti za serikali
waliamua kuzitafuna ambapo tatizo hilo limekuwa likijitokeza kila mwaka.
Serukamba akizungumza na wakuu wa
idara, wahasibu na watendaji wa vijiji na kata leo alisema Halmashauri ya
Wilaya ya Iramba ndio inayoongoza kati ya halmashauri saba za Mkoa wa Singida
kwa watumishi wake kukusanya fedha na kuzitafuta bila kuzipeleka benki.
"Mumeenda kwenye masoko
wananchi wema wamelipa ushuru na kodi lakini mtumishi tuliokupa jukumu la
kukusanya fedha baada ya kuzikusanya badala ya kuzipeleka benki unaamua
kuziweka mfukon maana yake tumekupa mtaji hili jambo haliwezekani,"
alisema.
Alisema katika kipindi chake akiwa
Mkuu wa Mkoa wa Singida kama kuna mtumishi anadhani hawezi kukusanya fedha za
serikali na kuzipeleka benki au halmashauri
basi aache kazi hii haraka.
Serukamba alisema katika ufisadi
huu kuna mambo mawili yanajitokeza inawekezekana kuna njama kati ya wakuu wa
idara na wakusanyaji ambapo fedha hizo zikikusanywa wanagawana na hivyo
serikali kukosa mapato.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Iramba,
Suleiman Mwenda, alisema tatizo hili limekuwa sugu katika wilaya hii ambapo
mwaka jana watumishi na mawakala walikuwa wanadaiwa zaidi ya Sh.millioni 200
lakini mwaka huu deni limeongezeka na kufikia zaidi ya Sh.milioni 300.
Mwenda alisema wakuu wa serikali
walishafika katika wilaya ya Iramba akiwamo Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa ambao
waliagiza fedha hizo zilizotafunwa na watumishi zirejeshwe lakini utekelezaji
wake umekuwa hafifu.
"Jambo hili limekuwa la muda
mrefu, mwaka jana watendaji walikuwa wanadaiwa zaidi ya Sh.milioni 200 pamoja
na serikali kuchukua hatua kwa watumishi waliohusika cha kushangaza ufujaji
umeongezeka na kufikia Sh.milioni 300 sasa," alisema.
Baada ya maelezo hayo ya Mkuu wa
Wilaya, Mkuu wa Mkoa alianza kusoma majina ya watumishi na mawakala wanaodaiwa
mamilioni hayo ya fedha na kila mmoja kutakiwa kujieleza lini atalipa deni
lake.
Hata hivyo, Serukamba alishtuka
maelezo ya utetezi yaliyokuwa yanatolewa na wadaiwa na kubaini kuna mchezo
mchafu (njama) iliyokuwa imetengenezwa kati ya wadaiwa na watumishi wa idara ya
fedha.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa
alimua kuwagiza watumishi wa idara ya fedha kuwafuatilia wadaiwa wote na fedha
hizo kuzirejesha ndani ya siku saba na kuahidi kufikia katika wilaya hiyo siku
ya Jumatatu ya wiki ijayo kuangalia kama fedha hizo zimerejeshwa.
Aisha, alimwagiza Mkuu wa Wilaya na
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Michael Matomora kufuatilia
suala hilo ili fedha hizo zirejeshwe ndani ya siku saba.
No comments:
Post a Comment