Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akizungumza wakati wa kikao cha Menejimenti kwa lengo la kujadili Mpango Mkakati wa kuhakikisha agizo la kila mwananchi anakata bima ya Afya ya CHF iliyoboreshwa kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa mkoa huo Agosti 24, 2022.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba ameagiza kuanza
kutekelezwa kwa agizo lake la kuhakikisha kila mwananchi Mkoani hapo anakuwa na
bima ya Afya ya CHF iliyoboreshwa kama hatua moja wapo ya kupambana na adui
maradhi.
Akiongea wakati wa kikao cha
Menejimenti kilichofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa ofisi hiyo
Serukamba amewataka wataalamu wa Idara ya Afya kuanza mara moja kutambua Kaya
zote ambazo zitahusika kwenye ukataji wa Bima ya Afya.
Aidha RC Serukamba amesema wataalamu
hao pamoja na utambuzi wa Kaya waendelee kutoa elimu na uhamasishaji juu ya Bima hiyo kwa wananchi
ambapo ameahidi kuzunguka Kata zote 136 za Mkoa wa Singida ili kuhamasisha
wananchi na viongozi mbalimbali lengo likiwa ni kupata Bima hiyo.
Lengo la kikao hicho ni kuandaa mkakati
wa namna ya kuhakikisha kila mwananchi mkoani humo anapata Bima ya Afya ili
waweze kufaidi uwepo wa vituo vya Afya na Zahanati ambazo zimejengwa maeneo
mbalimbali Mkoani hapo.
RC Serukamba amesema ili Mkoa uweze
kuinuka ki uchumi unahitaji kuwa na watu wenye Afya Bora ambayo itapatikana kwa
kila mtu kuwa na Bima ya Afya.
Amesema Mkoa inakadiriwa kuwa na
Kaya laki tatu (300,000) na endapo kila mwananchi atachangia Bima ya Afya ya SH.30,000
kwa mwaka Mkoa utapata zaidi ya Bilioni 9 ambapo bajeti ya dawa kwa mwaka ni kiasi cha Bilioni 8 hivyo hakutakuwa
na upungufu wa dawa vifaa tiba na vitenganishi.
Hata hivyo RC Serukamba amesisitiza
miradi mbalimbali ya kilimo isimamiwe vizuri na iweze kutumika kuleta matokeo
chanya kwa wakulima na wananchi kwa ujumla.
Akitolea mfano Skimu ya Itagata
iliyoko Halmashauri ya Itigi Wilayani Manyoni ambayo Serikali imetumia
fedha nyingi kiasi cha Milioni 735 na
ilitegemewa kuhudumia wakulima 209 ambapo kwa sasa ina hudumia wakulima
wachache na wengine waliendelea kuhodhi maeneo bila kuyatumia.
No comments:
Post a Comment