Wednesday, August 10, 2022

Mwenge wa Uhuru 2022 umezindua rasmi Daraja la Mawe lenye urefu wa mita 30 na upana wa Mita Nane wilayani Mkalama

 

Daraja la mawe lenye urefu wa Mita 30 na upana wa Mita nane (8) lililojengwa katika Kata na  Kijiji cha Miganga kilichopo Tarafa ya Nduguti Wilaya ya Mkalama.

Akiongea kabla ya kuzindua Daraja hilo Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Sahili Nyanzabara Gerurama amewataka Wahandisi kuendeleza Teknolojia hiyo ya mawe na wengine waige kwakuwa linatumika kiasi kidogo cha fedha ikilinganishwa na mengine yanayojengwa kwa zege na nondo.

Aidha amewataka wananchi kulitunza daraja hilo kwa kuondoa uchafu na kulinda vyuma visiibiwe ili kutorudia kwa changamoto ya upimaji wakati wa mvua kama ilivyokuwa mwanzoni.

Ukaguzi ukiendelea juu ya daraja hilo

Hata hivyo amewataka Wahandisi wa TARURA ambao ndio wasimamizi wa Ujenzi wa daraja hilo kuweka viakisi mwanga ili kuzuia ajali ambazo zinaweza kutokea wakati wa usiku.

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Sophia Kizigo alieleza umuhimu wa daraja hilo ambapo alieleza kwamba wananchi wa Kata ya Miganga walikuwa hawawezi kwenda Hospitali ya Wilaya kwa sababu ya maji yaliyokuwa yakisababisha barabara kutopitika kwa urahisi.

DC Kizigo amesema daraja hilo litawasaidia watu wa  Nduguti Nkinto, Miganga  na Nduguti katika shughuli zao za kibiashara na kijamii.

Kwa upande wake Mhandisi wa TARURA wilaya ya Mkalama  Mang'ara Magoti Maziku amesema Ujenzi wa daraja hilo umegharimu Tsh. Milioni 180.5 na kuokoa TSH.Milioni 639.4 kwa kuwa kama lingejengwa  kwa zege na nondo lingegharimu TSH.Milioni 820.

 Mhandisi Magoti amesema fedha hizo zimetolewa na Serikali kupitia fedha za mfuko wa Jimbo kwa mwaka 2021/22 na unatekelezwa na Mkandarasi Chase Investment  wa Mwanza na kazi zilizopangwa ni kuchimba kupanga mawe kusuka chuma kumwaga zege na kujenga mawe.

Ukaguzi ukiendelea ndani ya daraja hilo

Mwisho

No comments:

Post a Comment