Monday, July 18, 2022

RAS Singida awatembelea wakufunzi wa Sensa ahimiza umakini katika kazi.

 

Makarani wa Sensa Mkoani Singida wametakiwa kuongeza umakini wakati wa kufanyika kazi  madodoso kwa kuzingatia mila na desturi za jamii husika  ili kuepuka vikwazo vinavyoweza kujitokeza wakati wa kuendesha zoezi hilo.

Akiongea na wakufunzi hao leo wakati wa mafunzo hayo  ya Sensa  katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha ufundi stadi VETA Mkoani hapa Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Mwl. Doroth Mwaluko amesema pamoja na kujua namna ya kuuliza maswali lakini lazima saikolojia itumike kwa sababu bado jamii za watu wa Mkoa huo zinaishi kutokana na mila na desturi.

"Wapo watu ambao hawapendi kutoa taarifa zao za ndoa mfano swala la ndoa mara nyingi ni siri za familia hivyo unaweza kukosa majibu yaliyotarajiwa, ni lazima kutumia saikolojia na kuangalia mambo ya mila na desturi za maeneo husika katika kuuliza maswali" Alisema

Hata hivyo Mwaluko amewataka wakufunzi hao kuwa na uvumivu mkubwa na kutumia vizuri nafasi waliyopata  kwa kuwa taifa limewaamini kwamba wana uwezo wa kukamilisha zoezi la Sensa ya watu na makazi.

Awali mratibu wa Sensa Mkoa wa Singida Neing'oya Kipuyo amesema mafunzo hayo ni ngazi ya pili ya Mkoa ambayo yalianza tarehe 6 Julai na yatahitimishwa Julia 26 watakuwa tayari kwenda  kuwafundisha Makarani ngazi ya Kata na Tarafa.

Mratibu huyo ameeleza kwamba Mkoa wa Singida utakuwa na jumla ya Makarani na wasimamizi 542 ambao ndio watakaoshughulika na zoezi lote la Sensa.

Alisema  Sensa ya watu na makazi ina madodoso manne ambayo ni dodoso la makundi maalum, ambalo linahusu ukusanyaji wa taarifa za makundi ambayo hayawezi kuhesabiwa na madodoso ya kawaida.

Kipuyo aliendelea kueleza kwamba lipo dodoso la jamii ambalo linajazwa ndani ya siku mbili kabla ya siku ya Sensa wakati Karani akiwa analitambua eneo lake la kuhesabiwa watu ambapo anakusanya taarifa zinazohusu mambo ya kijamii kama mashule  zahanati masoko na huduma za kifedha.

Dodoso jingine  ni la majengo ambalo taarifa hukusanywa  kuhusu majengo yote ya makazi na yasiyo ya makazi,  na dodoso la anwani za makazi ambalo linalenga kukusanya taarifa mbalimbali za anwani za makazi kama majengo nyumba na viwanja.

Amesema tayari wameshakamilisha madodoso matatu kati ya manne na kundi hilo linatakiwa kuanza mafunzo ya vitendo siku ya tarehe 19 Julai 2022.

Matukio katika picha

Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Mwl. Doroth Mwaluko akiongea na wakufunzi wakati wa mafunzo ya Sensa  katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha ufundi stadi VETA Mkoani Singida.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Mwl. Doroth Mwaluko akiohojiana na mkufunzi wakati wa mafunzo ya Sensa kwa vitendo.



Mafunzo yakiendelea

Mratibu wa Sensa Mkoa wa Singida Neing'oya Kipuyo akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa mafunzo ya Sensa yanayofanyika katika ukumbi wa Veta  mkoani Singida.





Afisa Maendeleo Mkoa wa Singida akiwa katika mafunzo ya zoenzi la Sensa mkoani Singida

Mafunzo yakiendelea

No comments:

Post a Comment