Halmashauri za Wilaya zimetakiwa kuimarisha vyanzo vya mapato
na mifumo ya ukusanyaji fedha ikiwa ni pamoja na kubuni miradi mipya itakayoongeza
mapato ya Serikali.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa
alipokutana na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba katika ukumbi wa
mikutano wa Halmashauri hiyo.
Amesema wapo watumishi
na mawakala ambao wamepewa kazi ya ukusanyaji wa mapato lakini hawapeleki fedha
Benki na wengine kuzitumia kwa matumizi yao binafsi hivyo kuwataka viongozi
kuwachukulia hatua wote waliosababisha
upotevu wa fedha hizo.
"Mnaweka mawakala kwenye ukusanyaji wa mapato ambao
hamna mikataba nao, niwaombe Madiwani itisheni hiyo mikataba muikague na
wachukulieni hatua watumishi ambao
wamekula Milioni 300" alisema.
Hata hivyo ametoa onyo kwa Maafisa Tehama ambao wanaingilia
mifumo ya ukusanyaji wa fedha ili kukwepesha fedha kutosomeka kwenye mifumo
hivyo na kusababisha upotevu wa fedha kupitia mashine za Posi.
Kwa upande wake Naibu Waziri ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za mitaa Dr. Festo John Dugange amesema TAMISEMI ni Wizara ya wananchi hivyo watumishi
wakisimamia taratibu zinazotakiwa Serikali itakuwa imefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 70.
Dr. amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba Tamisemi wamepokea
hizo changamoto na watazifanyia kazi ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata
huduma kama ilivyokusudiwa.
Aidha amewataka watumishi kuachana na vitendo vya kinyume na
maadili kwa sababu kwa yeyote atakayehujumu au kufanya jambo kinyume atakamatwa
kwa kuwa Serikali ni kama hewa inapatika popote alisisitiza Naibu Waziri.
Hata hivyo Naibu Waziri amekiri kuwepo kwa changamoto katika
ukusanyaji wa mapato ya ndani jambo ambalo amesema wamelipokea na wanaendelea
kulifanyia kazi ili kurekebisha hali hiyo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment