Thursday, May 19, 2022

Watoto 286,736 kupatiwa chanjo ya Polio Singida

 

Mkoa wa Singida unatarajia kutoa chanjo ya Polio kwa watoto 286,736 wenye umri wa Miezi sifuri mpaka 59 katika Halmashauri zote za Mkoa huo ifikapo mwishoni mwa mwezi wa Sita mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa huo Dk. Binilith Mahenge wakati akizindua kampeni ya utoaji wa chanjo ya Polio iliyofanyika Iguguno Mkoani hapo huku akiwataka wananchi kuwapeleka watoto wao wakapate chanjo.

Aidha RC Mahenge ametoa wito kwa Wakurugenzi na wakuu wa Wilaya kuhakikisha malengo yanafikiwa kwa kuzingatia malengo ya kila Wilaya ili kujenga Taifa lenye watu wenye Afya njema.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge (wa katikati) akizindua kampeni ya utoaji wa chanjo ya Polio iliyofanyika Iguguno Mkoani Singida. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo na kulia ni Mganga Mkuu wa Mkoa  DK. Victorina Ludovick

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo amesema kazi yake kama Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ni kuhakikisha watu wanakuwa salama na wenye uwezo wa kuzalisha hivyo ulinzi huo utaanzia kwenye kuboresha Afya za watoto kwa kuwapatia chanjo.

Amesema Taifa lenye mafanikio ni lenye kuwajali watu wake wakiwemo watoto kwa kuwa ndio viongozi na matajiri wa kesho hivyo kwa nafasi yake amewataka wazazi kuwapeleka watoto wakapate chanjo kwa kuwa haina madhara hata kwa mtoto ambaye alishachomwa wakati alipozaliwa.

Awali akitoa taarifa kuhusu lengo la chanjo hiyo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida DK. Victorina Ludovick amesema ni kwa watoto wenye miaka sifuri mpaka miezi 59 ili kuwazuia athari za mfumo wa fahamu unaosababishwa na polio.

Amesema ugonjwa huo hauna kinga ila unaweza kuzuiliwa kwa kupata chanjo ya polio kwa njia ya matone Ugonjwa ambao mtu huweza kupata kwa kunywa au kula kinyesi.

Ludovick amesema maandalizi yote yamefanyika kwa kupata vifaa na kuandaa vituo mbalimbali. 

Amesema zoezi la Chanjo litatolewa kwa njia mbalimbali zikiwemo nyumba kwa nyumba huduma ya Mkoa na katika vituo mbalimbali vya Afya.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge (wa katikati) akishiriki moja ya zoezi la kampeni ya utoaji wa chanjo ya Polio ikiwa ni ishara ya uzinduzi rasmi iliyofanyika katika Wilaya ya Iguguno Mkoani Singida Mei 19, 2022

No comments:

Post a Comment