Dhamira ya kuondoa uhaba wa mafuta nchini na kupambana na changamoto ya upatikanaji wa mbegu Bora za alizeti imeendelea kutumika kufuatia Wawekezaji kuonesha nia ya kuwekeza katika kujenga kiwanda cha mafuta ya alizeti na uzalishaji wa mashamba ya utafiti na uzalishaji wa mbegu.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge amebainisha ukweli huo leo alipokuwa akiongea na Viongozi wa Kampuni ya Alizeti Qwanza moja kati ya makampuni Export Treder wakitaka kupata maeneo ya uwekezaji Mkoani hapa.
Kampuni hiyo imebainisha kwamba inahitaji ekari 100 kwa ajili ya Ujenzi wa kiwanda kwa ajili ya uzalishaji wa mafuta na ekari 2000 kwa ajili ya utafiti na uzalishaji wa mbegu.
Aidha msemaji wa Kampuni hiyo amesema kwamba wanatarajia kufanya kilimo cha Umwagiliaji ambacho kitakuwa kikifayika Mara mbili kwa msimu ili kupata mazao ya kutosha.
Kampuni hiyo imewekeza katika nchi 56 za Afrika na duniani na kwa Tanzania imekuwa ikifanya Biashara ya ununuaji wa mazao na uzalishaji wa mpunga Wilayani Mbarali wakati Zanzibar ikiwa inazalisha sukari kwa kushirikisha wakulima wadogo wa miwa.
Akijibu taarifa yao RC Mahenge alisema kwamba Mkoa wa Singida yapo maeneo yametengwa kwa ajili Ujenzi wa viwanda vikubwa na vidogo na maeneo ya mashamba katika Wilaya ya Ikungi, Mkalama na Singida Dc.
Hata hivyo RC Mahenge ameeleza kwamba kwa sasa kuna changamoto ya uzalishaji wa mafuta duniani hivyo wakitumia fursa ya upatikanaji wa mashamba na kwa kushirikiana na wakulima wa Mkoa huu wana uhakika wa kupata soko kubwa na la uhakika.
RC Mahenge amewaagiza Wakurugenzi kutoa ushirikiano mkubwa kwa Wawekezaji hao ikiwa ni pamoja na kuwapitisha katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji katika Halmashauri hizo.
"Singida ni katikati ya nchi na ni karibu na makao makuu ya Serikali, lakini pia zipo Barabara zinazo unganisha mikoa yote na baadhi ya nchi za jirani ambapo hali hiyo ambayo inaongea mahitaji ya bidhaa watakazozalisha" alieleza Mahenge.
No comments:
Post a Comment