Thursday, May 19, 2022

Mwili wa tatu wa moja ya watenda kazi katika Mgodi wa Senkeke wapatikana

Serikali  imefanikiwa kupata  Mwili wa tatu wa moja ya watenda kazi katika Mgodi wa Senkeke uliopo Mkoani Singida  baada ya waokoaji kumtafuta kwa kipindi cha Siku mbili na kumkuta akiwa amenasa katika miamba ndani ya maji.

Akiongea na waandishi wa habari jana ofisini kwake Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Binilith Mahenge amelipongeza Jeshi la zimamoto kwa juhudi walizofanya mpaka kupata Mwili wa kijana huyo aliyetambuliwa kwa jina la Pascal Hendry mwenye umri wa  miaka 25 ambaye alikuwa kati ya watenda kazi watatu waliozama kwenye maji  katika Mgodi huo baada ya gema lililotumika kuegeshea uchanja waliokuwa wakitengeneza kwa ajili ya kuvuka upande wa pili kuvunjika na kutumbukia majini.

Aidha RC Mahenge  ametoa maagaizo kwa Kaimu Kamishna wa Madini Mkoani hapo kufanya uchunguzi katika migodi yote ili kutambua changamoto za kiusalama zinazokabili migodi hiyo na kuzitafutia ufumbuzi.

Aidha Mahenge ameagiza kila mwekezaji katika kila Mgodi kuhakikisha anakuwa na vifaa vya uhakika na vya kutosha vya tahadhari na uokoji katika maeneo hayo kama njia ya kujikinga na majanga  hayo yasiweze kutokea kwa Mara nyingine.

Hata hivyo RC Mahenge ameagiza kufungwa kwa muda shimo namba 100A katika Mgodi huo ambapo ajali ilitokea mpaka wataalamu watakapo jiridhisha kwamba maeneo hayo ni salama kwa watu kufanya kazi huku akimtaka Kamishna kuandaa ziara ambayo itahusisha kamati ya usalama ya Mkoa kukagua migodi yote ili kujionea kama hatua ya  maelekezo hayo yametekelezwa.

Kwa upande wake Kamishna wa Madini Chone Lugangizya Malembo ameahidi kutekeleza maagaizo hayo haraka iwezekavyo huku akiendelea kuwashukuru wadau mbalimbali ambao wamesaidia kupatakiana kwa mwili wa mtendaji kazi huyo.

Awali akitoa taarifa ya uokoaji  Devota Migawa, Jeshi la zimamoto ameomba uwepo wa utaratibu wa utoaji taarifa kwa wakati ili kunusuru Maisha ya watu na Mali zao.

No comments:

Post a Comment