Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoani Singida wametakiwa kuimarisha ulinzi katika vituo vyao vya kupoozea Umeme kikiwemo cha mkoani hapo kama tahadhari ya kupambana na waharibifu wa miundombinu hiyo.
Kauli hiyo imetolewa tarehe 17.05.2022 na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge alipotembelea Kituo hicho na kujionea walinzi wakiwa wachache ndio akabaini kwamba usalama wa eneo hilo la uwekezaji pamoja na wafanyakazi wake haujitoshelezi.
Akiwa katika ziara hiyo iliyowashirikisha vyombo vyote vya usalama vya Mkoa huo RC Mahenge akasema uwekezaji huo ni mkubwa hivyo unahitaji ulinzi wa kutosha huku akiwataka Tanesco kushirikiana na Jeshi la Polisi kabla ya kupata walinzi wao ili kuimarisha hali ya usalama katika eneo hilo.
Aidha amemtaka Meneja wa Tanesco Singida kutembelea Wilaya ya Mkalama Manyoni na Itigi kwa kuwa eneo hilo inasemekana Umeme unakatika Mara kwa Mara na kuleta kero kwa wafanyabiashara.
Akipokea maelekezo hayo Afisa usalama wa Shirika la Umeme Tanesco Devisi Mkuche amesema tayari wameandaa mkakati wa kukabiliana na hali ya kuimarisha usalama katika Mradi huo ambao tayari kulishaanza kuwa na wezi wa vitu vidogovidogo.
Amesema wameendelea kuwa na ushirikiano wa karibu na Jeshi la Polisi ili kusaidia kukabiliana na hali hiyo wakati Shirika likiendelea kuandaa Mkakati wa kupata walinzi wake kupitia mashirika mbalimbali ya ulinzi.
Hata hivyo Mkuche ameeleza kwamba bado Mkandarasi wa mitambo hiyo hajakabidhi kwa Shirika jambo ambalo ililazimu swala la ulinzi kubaki mikononi mwa Mkandarasi huyo.
Kwa upande wake Meneja wa Mradi huo Deogratius Nyantumbaga amesema Mradi huo umeshakamilika kwa upande wa Singida na tayari wameshawasha Umeme hivyo wanategemea kukabidhi kwa Tanesco mwishoni mwa mwezi ujao.
No comments:
Post a Comment