Taasisi zisizo za Serikali ambazo zipo ndani ya Manispaa ya Singida zimetakiwa kutoa maelezo juu ya kutokuwepo kwa vibao vya Anwani za Makazi na postikodi katika maeneo hayo wakati yalikuwa ndio makubaliano kwa taasisi zote kufanya hivyo.
Maelekezo hayo yametolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilithy Mahenge alipofanya ziara ya kukagua uwekaji wa Anwani za Makazi na postikodi katika Kata za Majengo na Mwankoko Manispaa ya Singida Mkoani hapa baada ya kupata taarifa kutoka kwa Mtendaji Kata hiyo kwamba taasisi zilizobaki ni zile binafsi zikihusisha Misikiti na Makanisa.
"Mkurugenzi waiteni wote wenye taasisi binafsi waeleze kwa nini wanachelewesha zoezi la Anwani za Makazi kwa kutoweka vibao vinavyotambusha maeneo yao?, nataka ifikapo alhamisi tarehe 12 Mei 2022 nipate taarifa ya uwekaji wa vibao katika Taasisi hizo" Alisema Rc Mahenge.
Aidha pamoja na changamoto hizo RC Mahenge ameipongeza Manispaa hiyo kwa kutekeleza kwa usahihi zoezi la uwekaji wa namba za nyumba na vibao elekezi vya Barabarani hivyo kuwataka kuhakikisha wanamalizia sehemu chache zilizobaki kabla ya Siku ya tathmini ambayo ni tarehe 12 Mei 2022 alibainisha RC Mahenge.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida Jeshi Lupembe ameahidi kutekeleza maagaizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa ikiwemo kurekebisha baadhi ya vibao elekezi na kuwaita wenye taasisi binafsi kujua kwanini hawajaweka vibao vya Makazi na wanaviweka Siku gani.
Jeshi ameongeza kwamba endapo kutatokea ugumu wowote katika kufanikisha zoezi hilo Halmashauri italazimika kuweka vibao vyenye ubora hafifu ili kuondoa dosari katika zoezi hilo ambapo watalazimika kubadilisha wenyewe baadae.
Ziara hiyo iliwashirikisha viongozi mbalimbali wa Mkoa, Wilaya na Halmashauri ya Manispaa ya Singida na inategemewa kufanyika tena Siku ya tareh 12 Mei 2022 asubuhi katika Wilaya ya Singida Vijijini kabla ya tathmini.
No comments:
Post a Comment