Madiwani wa Kata za Manyoni Mkoani Singida Wametakiwa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa zoezi la uwekaji wa Anwani za Makazi na Posti Kodi ili kutatua changamoto mbalimbali ambazo zimesababisha zoezi hilo kushindwa kukamilika kwa wakati katika Kata hizo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Binilith Mahenge akiwa katika Kikao kazi na Madiwani kilichofanyika ukumbi wa Halmashauri ya Manyoni ambapo amesema kusuasua kwa zoezi la uwekaji wa anwani za Makazi Wilayani hapo limetoka na ushikishwaji mdogo baina ya Watendaji, Madiwani pamoja na wakuu wa Idara.
Kufuatia kauli hiyo RC Mahenge amewataka wakuu wa Idara wote kuwa miongoni mwa kamati za utekelezaji wa zoezi hilo na kutumia muda wa Siku mbili kuhakikisha vibao vyote vinawekwa na nyumba zote zinabandikwa namba au kuandikwa kwa mkono.
"Haiwezekani muda wote tunasubiria stika za kubandika mlangoni ambapo nyumba zaidi ya 42800 zilizowekwa namba hazifiki hata nusu yake jambo ambalo kama mngeandika kwa rangi au makapen mngekuwa mmeshamaliza, naagiza ndani ya Siku mbili kuanzia leo kazi hii iwe imekamilika" Alifafanua RC Mahenge.
RC Mahenge amesema ikifika tarehe 13 kazi hiyo haijakamilika hata sita kuwasimamisha kazi watumishi ambao wamesababisha uzembe huo huku akiwataka Polisi Magereza na Askari wanyamapori kuwasiliana na Mkurugenzi ili magari yao yatumike katika usambazaji wa vibao ambayo vimekamilika lakini havijafikishwa sehemu zinazostahili.
Hata hivyo RC Mahenge amewataka watumishi hao kutojiingiza katika mambo ya siasa badala yake watekeleze majukumu yao kwa ufasaha huku akiwataka madiwani kushiriki shughuli zote za maendeleo katika maeneo yao ili kusaidia kuleta mabadiliko ya maisha kwa wananchi wao.
Sambamba na hilo RC amekemea vikali tabia za watumishi wa umma kutumia vilevi kulikokithiri akioanisha na utendaji kazi usio ridhisha wa watumishi mbalimbali wa Halmashauri hiyo.
Wilaya ya Manyoni imekuwa na changamoto katika uwekaji wa anwani za Makazi mijini na Vijijini kutokana na kufanya kazi bila ushirikiano na kutowajibika kikamilifu kwa waliopewa dhamana ya kuongoza jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma mipango ya Serikali Wilayani hapo alibainisha RC Mahenge.
No comments:
Post a Comment