Monday, May 09, 2022

Watendaji wa Makiungu, Mungaa Watakiwa kufanya "Data Cleaning" Katika zoezi la uwekaji wa Anwani za Makazi.

Watendaji wa Kata na Vijiji wametakiwa kufanya uhakiki wa namba za nyumba walizoweka  (data cleaning)  pamoja na vibao elekezi katika maeneo yao ya kazi  kabla ya kukamilisha na kukabidhi zoezi hilo kwa viongozi husika ili kuondoa dosari zilizojitokeza katika baadhi ya Kata wilayani Ikungi mkoani Singida.  

Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Tawala Mkoa huo Dorothy Mwaluko akifanya ziara ya kukagua utekelezaji wa zoezi la uwekaji wa  anwani za Makazi katika Kata za Makiungu, Mungaa na Siuyu katika Wilaya hiyo na kubaani changamoto ndogo ndogo zikiwemo uwekaji wa namba usiokuwa na Mpango mzuri pamoja na usimikaji wa vibao elekezi vyenye mbawa moja badala ya mbili.

 Akitoa majumuisho katika ziara hiyo amesema Wilaya  imefikia  hatua nzuri pamoja na uwepo wa changamoto chache zilizojitokeza ambapo amewataka Watendaji kuzikagua namba hizo na  kuziwasilisha kwa viongozi wao haraka ili kutafutiwa ufumbuzi wa haraka alieleza Dorothy Mwaluko.

Hata hivyo Mwaluko amewataka wananchi na wenyeviti wa vitongoji kuendelea kushirikiana na   waratibu wa anwani za Makazi ili kumaliza zoezi hilo kwa wakati.

Aidha, RAS akimalizia ziara yake katika kata hizo akawataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote kutumia muda uliobaki kujiridhisha na maeneo yaliokwisha tolewa taarifa kwamba yamekamilika  ili kujiridhisha ukamilifu wake.

Dorothy akaendelea kuwakumbusha Wakurugenzi hao kuhakikisha kila Taasisi zikiwemo mashule Misikiti, Makanisa na ofisi za watendaji kwamba zinakuwa na vibao vya anwani za Makazi.

Ziara hiyo iliwahusisha viongozi kutoka Jeshi la Magereza ngazi ya Mkoa, Jeshi la Uhamiaji Mkoa na Maafisa mbalimbali kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Zoezi hilo la kukagua utekelezaji wa uwekaji wa anwani za Makazi  ulifanyika pia katika Wilaya ya Manyoni na Halmashauri ya Itigi ambapo kamati ya ufuatiliaji kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo iliongozwa na Mshauri wa Jeshi la Akiba, Mkuu wa Takukuru pamoja na Mratibu wa Anwani za Makazi Mkoa ambapo iliwasisitiza Watendaji kuongeza kasi ya utekelezaji ili kufikia lengo tarajiwa pamoja na kuboresha namba za anwani za makazi na usimikaji wa vibao elekezi.

Zoezi likiendelea katika Halmashauri ya Igiti wilayani Manyoni

No comments:

Post a Comment