1. Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorthly Mwaluko akiwa kwenye ziara ya kutembelea miradi ya ujenzi wa vyumba vitano (5) vya madarasa katika shule ya Sekondari Ibaga iliyopo Kata ya Ibaga mkoani Singida
WATENDAJI wa Serikali katika ngazi ya Kata, Tarafa na vijiji
mkoani Singida wametakiwa kutumia muda wao mwingi katika kusimamia ujenzi wa
vyumba vya madarasa unaoendelea katika maeneo mbalimbali mkoani hapa ili
kufanikisha ujenzi huo kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.
Mkoa wa Singida umepokea fedha za UVIKO-19
kiasi cha Shilingi Bilioni 13.24 kwa upande wa elimu ili kujenga vyumba vya
madarasa 632 ambapo vyumba 330 ni kwa ajili ya shule za sekondari na 330 shule
za msingi pamoja na mabweni mawili kwa ajili wenye mahitaji maalum ikiwa ni
matarajio ya Serikali kwamba fedha hizo zitasimamiwa na kukamilisha ujenzi huo.
Kauli hiyo imetolewa Novemba 29,2021 na
Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko wakati akikagua miradi
mbalimbali ya ujenzi wa vyumba hivyo katika Wilaya ya Mkalama ambapo
amebainisha kwamba hali ya ujenzi inaendela vizuri na vyumba vingi vikiwa
vimefikia katika hatua ya lenta na vingine vikisubiri kupauliwa.
RAS amewataka viongozi mbalimbali wa
Serikali wakiwemo watendaji wa vijiji, Kata na Tarafa kuhakikisha haipiti siku
bila kujua kinachoendelea katika miradi hiyo ambayo inatakiwa kukamilika kabla
ya Desemba 15, mwaka huu.
Ziara hiyo ya RAS imehusisha viongozi
mbalimbali wa Wilaya ya Mkalama ambapo walitembelea miradi katika shule ya
Ibaga Kata ya Ibaga ambapo kunajengwa vyumba vitano vya madarasa, Shule ya
Sekondari Nduguti kunakojengwa vyumba viwili, Shule ya Sekondari Gunda Kata ya
Ilunda kunakojengwa chumba kimoja, Shule ya Sekondari Grace Mesaki kunakojengwa
chumba kimoja, Kikhonda Sekondari kwenye ujenzi wa vyumba vitatu (3) na Shule
ya Sekondari Iguguno kunakojengwa vyumba vinne vya madarasa .
Akiwa katika miradi hiyo, Dorothy Mwaluko
ametuma ujumbe kwa wakuu wa shule zote mkoani Singida zenye miradi inayotumia
fedha za UVIKO-19 kuhakikisha wanajenga kwa kufuata michoro iliyokubalika na
kuhakikisha kwamba wanafanya mawasiliano ya karibu na wahandisi wa halmashauri
za wilaya zao endapo kuna umuhimu wa kufanya hivyo ili kulinda ubora na viwango
vilivyotajwa na wataalamu hao.
Aidha, RAS akawataka viongozi kuhakikisha
wanazishirikisha kamati za ujenzi wa madarasa na kamati za mapokezi ya vifaa
vya ujenzi, kiasi cha fedha zilizokuja na namna ya matumizi ya fedha hizo kama
sehemu ya kuweka uwazi na kutengeneza dhana ya ushirikishwaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkalama,
Sophia Kizigo amesema wilaya imepokea fedha kwa ajili ya ujezi wa vyumba vya
madarasa 63 na ya shule shikizi 16 ambazo kwa jitihada wanazofanya vyote
vitakamilika ndani ya wakati.
DC Sophia amebainisha kwamba, hali ya
ujenzi kwa sasa inaendelea vizuri baada ya kumaliza changamoto ya upatikanaji
wa vifaa vya ujenzi ambavyo amesema vilikuwa havipatikani kwa kuwa zoezi la
ujenzi wa vyumba vya madarasa unafanyika nchi nzima, hivyo kusababisha
changamoto za upatikanaji wa vifaa hivyo.
Amesema, kwa sasa wilaya imeshanunua vifaa
vyote vinavyohitajika katika ujenzi huo ambapo amebainisha kwamba asilimia 85
ya majengo yamefikia hatua ya kufungwa lenta wakati asilimia 15 vinafungwa
mkanda wa katikati ili kuondoa nyufa zinazoweza kutokea.
DC amefafanua kwamba, mbao zitakazotumika
kwa wilaya nzima tayari zimeshafika kilichobaki ni kuzisambaza kwenye shule
mbalimbali na mpaka kufikia Novemba 30, 2021 jioni mabati nayo yatakuwa
yamefika.
Wakimalizia ziara hiyo katika shule Sekondari
Iguguno, DC Sophia amezitaka kamati za mapokezi na za ujenzi kujipanga kupokea
vifaa hivyo ambapo watatakiwa kuongeza usimamizi ili kupata thamani ya fedha
zilizotumika.
Mwisho DC Kizigo akamshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo
katika Wilaya ya Mkalama jambo ambalo amesema limeondoa kabisa changamoto ya
uhaba wa madarasa.
No comments:
Post a Comment