Thursday, November 11, 2021

Singida ya Pili kwa Usimamizi Mahiri wa Miradi ya Maendeleo

Mkoa wa Singida umekuwa wa pili Kati ya mikoa 31 za Tanzania Bara na Visiwani kutokana na usimamizi mahiri wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyokaguliwa na kuzinduliwa wakati wa  Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2021.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge ametoa pongezi kwa viongozi mbalimbali, wahandisi na wananchi wa Mkoa huo kwa kusimamia miradi kwa ukaribu hadi Mkoa kuingia katika nafasi ya tatu Bora .

Akiongea kwa nyakati tofauti hivi karibuni alipokuwa anakagua miradi ya Ujenzi wa vyumba vya madarasa unaoendelea mkoani hapa Dkt. Mahenge ameendelea kutoa pongezi kwa viongozi na wananchi hao na kuwataka kuendelea  kusimamia miradi inayoendelea kwa umakini mkubwa.

Dkt. Mahenge amebainisha kwamba Mkoa wa Singida umekuwa wa pili wakati Mkoa wa Shinyanga ukiwa nafasi ya kwanza na nafasi ya tatu kuchukuliwa na Mkoa wa Mwanza.

Amesema jumla ya miradi ambayo ilikaguliwa na Mwenge wa Uhuru Mkoani Singida  iligharimu kiasi cha sh.Bilioni 8.1  ambacho kimetumika katika miradi 55 ya maendeleo kwa Mkoa mzima.

“Jumla ya miradi 55 inayohusu TEHAMA, Elimu, Afya, Mazingira, Maji, Biashara, Barabara, programu za Rushwa, VVU/UKIMWI, Malaria na mapambano dhidi ya dawa za kulevya zilitembelewa” amesema Dkt. Mahenge

Aidha Mbio za Mwenge mwaka 2021 miradi mipya 9 ilizinduliwa, miradi  miwili ilifanyiwa ufunguzi, sita(6) iliwekewa jiwe la msingi na 36 ilikaguliwa.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amewaasa wataalamu kuendelea na kasi hiyo ya kusimamia miradi ya Serikali vizuri huku akiwakumbusha viongozi mbalimbali kwamba watapimwa uwezo wao kwa kuangalia ubora wa kazi zilivyosimamiwa.

No comments:

Post a Comment