Tuesday, October 05, 2021

Wananchi Singida washauriwa kufanya mazoezi na kula mlo kamili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza

Wananchi wa Mkoa wa Singida wameshauriwa kufanya mazoezi na kuendeleza kula mlo kamili ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kuimarisha afya ya akili na mwili.

Akizungumza baada ya kukutana na mwandishi wetu katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Singida Afisa Lishe Mkoa Bi. Teda Sinde amesema ni muhimu makundi matano ya chakula yazingatiwe wakati wa ulaji na kufanya mazoezi ili kujenga afya Bora.

"Kwa Mkoa wa Singida makundi haya ni uwele, mahindi, mchele, mtama, ulezi na  kundi la pili ni la mikunde na vyakula vyenye asili ya wanyama kama maziwa, nyama, mayai, samaki, na dagaa kundi la tatu matunda na mboga na kundi la tano mafuta, sukari na asali" Alisema Teda.

Aidha amebainisha kwamba kundi la tano ambalo ni la sukari, mafuta na asali linatakiwa kutumika kwa kiasi kidogo ili kupunguza uzito mkubwa na mafuta mengi mwilini.

Bi Teda alimalizia kwa kutoa wito kwa vijana na wazee  kuhakikisha wanafuata utaratibu wa ulaji ili kuepusha magonjwa katika miili yao.

No comments:

Post a Comment