WASHAURI wa mambo ya fedha leo wamekutana
katika ukumbi wa ofisi za ukaguzi wa hesabu za serikali (NAO) Mkoani Singida kujadili
namna ya kutatua changamoto zinazosababisha upatikanaji wa hati chafu au zenye
mashaka kulingana na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
ya mwaka wa Fedha 2019/20 katika baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini.
Imeelezwa pamoja na mambo
mengine, lengo la kikao hicho ni kukubaliana na kuweka mikakati ya pamoja
itakayosaidia wakaguzi na wakaguliwa kutekeleza wajibu wa kisheria kwa namna
ambayo itaongeza tija na kuboresha utendaji.
Akizungumza wakati akifungua
kikao kazi hicho, Katibu Mkuu TAMISEMI Profesa Riziki Shemdoe alisema matokeo
ya ukaguzi huo hayakuwa ya kuridhisha kutokana na mwenendo usioridhisha wa Hati
za Ukaguzi zilizopatikana ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliotangulia wa
2018/19.
"Kumekuwa na poromoko la
halmashauri kupata hati safi na hii haikubaliki. Haiwezekani kuwe na poromoko
la hati safi kutoka halmashauri 176 mwaka 2018/19 hadi halmashauri 124 mwaka
2019/20...nahitaji kikao hiki kije na mkakati madhubuti na maazimio
yatakayosaidia kuleta maboresho stahiki," alisema.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo,
halmashauri zilizopata Hati Zenye Shaka ziliongezeka kutoka 9 mwaka 2018/19
hadi halmashauri 53 mwaka 2019/20, huku 8 zikijikuta zinapata Hati Chafu.
Alisisitiza kwa kuzitaka Mamlaka
za Serikali za Mitaa kupitia Waweka Hazina na Maafisa Masuuli kuwa makini
katika kipindi hiki wanapokwenda kufunga vitabu, kwa kuhakikisha zinajiepusha na
aina yoyote ya ubadhirifu na matumizi yasiyofaa ya fedha za umma ili kuepuka
hati chafu na zile zenye mashaka.
"Ni matumaini yangu baada ya
kikao hiki ambacho namuona mwakilishi wa Ofisi ya CAG, Mhasibu Mkuu wa
Serikali, Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa, Maafisa Masuuli na wadau wengine mliopo tuhakikishe tunajadili kwa kina
changamoto zote zilizojitokeza na kuhakikisha hazijirudii," alisema.
Aidha, Prof. Shemdoe alisisitiza
baada ya kikao hicho kilichofadhiliwa na USAID kupitia Mradi wa PS3+, Ofisi ya
Rais-TAMISEMI itakuwa tayari kutekeleza makubaliano yatakayofikiwa na kuratibu
utekelezaji wa yale yote yatakayopaswa kutekelezwa na Sekretarieti za Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa katika muktadha wa maboresho ya huduma bora kwa
wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali Divisheni ya Serikali za Mitaa, Benjamin Mashauri,
alibainisha sababu kubwa ya ongezeko la hati chafu na zile zenye mashaka kuwa
kubwa ni changamoto kwenye eneo la uandaaji wa Hesabu.
Pia Mashauri alisema eneo lingine
linalopelekea hali hiyo ni kwenye mapato ambayo pamoja na mambo mengine,
mengine hukusanywa lakini hayapelekwi benki wala kwenye mifumo stahiki.
Aliongeza kuwa changamoto
nyingine ni kwamba taarifa za kwenye vitabu haziendani na taarifa halisi za
mapato yanayokusanywa. Hali inayopelekea kiasi kikubwa cha matumizi ya Fedha za
Umma kujikuta zikifanyiwa matumizi bila ya kuwa na viambatanisho stahiki.
"Vilevile kuna masuala ya
changamoto za matumizi ya mifumo ya kisasa katika uandaaji wa hesabu kulingana
na Kanuni za Mfumo wa Kimataifa za uandaaji wa Hesabu za Taasisi za Umma., huko
nyuma tulikuwa na mfumo wa Epicor sasa ni Muce, hivi vyote visipozingatiwa
hupelekea matokeo ya uzalishaji huu wa hati chafu na zenye mashaka,"
alisema Mashauri.
No comments:
Post a Comment