Mkuu wa Mkoa
Singida Dkt. Binilith Mahenge (katikati) akikata utepe kuashiria ufunguzi wa
Zahanati ya Kijiji cha Maweni
wilayani Manyoni katika Hafla iliyofanyika kijijini hapo jana wakati
wa zaira yake ya kukagua miradi ya maendeleo. Wengine ni viongozi mbalimbali wa
wilaya hiyo.
MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith
Mahenge amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Maweni kilichopo wilayani Manyoni
mkoani hapa kwa hatua walioichukua ya ujenzi wa Zahanati ambayo inakwenda
kuondoa adha waliyokuwa wakiipata kwa kutembea umbali mrefu kufuata huduma za
matibabu maeneo ya mbali.
Dkt. Mahenge ametoa pongezi hizo jana
wakati akikagua miradi ya maendeleo wilayani Manyoni mkoani hapa leo ambapo pia
alipata fursa ya kuzungumza na wananchi.
"Hatua yenu mliyoichukua ya kuhamasishana na kupata Sh. 9 Milioni kwa
ajili ya kuanza ujenzi huu na kuungwa mkono na Serikali hadi kukamilisha ujenzi
wa zahanati hii mnastahili kupongezwa naomba na vijiji vingine viige mfano
huu,". alisema Mahenge.
Dkt. Mahenge alitumia nafasi hiyo
kuwapongeza viongozi wa chama na Serikali kwa wa wilaya hiyo kwa kufanikisha
kukamilisha ujenzi huo.
Mganga Mkuu wa Zahanati hiyo Furaha Mwakafwila
akitoa taarifa ya ujenzi wa Zahanati hiyo alisema itahudumia wakazi wa kijiji
hicho 3749 ambao wanaizunguka na kuwa gharaza zote za kukamilisha ujenzi huo
umegharimu zaidi ya Sh. 82 Milioni.
Akizungumzia kuhusu watumishi watakao
kuwa wakitoa huduma kwa wananchi katika Zahanati hiyo kwa maana waganga na
wauguzi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Melkizedek Humbe alisema
tayari wamepatikana na mmoja atafika hivi karibuni baada ya kumaliza masomo
yake mwezi huu kwa ajili ya kumsaidia aliopo wakiwepo wahudumu wa afya ya jamii
ambao wametakiwa kufika kuongeza nguvu ya kuhudumia wananchi.
Alisema katika bajeti ya mwaka wa
fedha unaokuja watatenga fedha kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa majengo mengine
ya Zahanati hiyo.
Katika hatua nyingine Dkt.Mahenge
alilipongeza Shirika la Compassion International Tanzania (CIT) kwa kuwawezesha vijana wajasiriamali
kutoka vikundi vituo vinne vya huduma ya mtoto na kijana Klasta wilayani humo
kwa kuwapa vifaa mbalimbali vya uzalishaji mali vyenye thamani ya zaidi ya
Sh.80. 4 Milioni.
Vikundi hivyo ni kutoka Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),
Kanisa la Moravian, Kanisa la Evangelist Assemblies of Gof (EAGT) na Kanisa la
Tanzania Assemblies of God (TAG)
Meneja wa Shirika hilo Kanda ya
Kati, Emmanuel Pando alisema shirika la
CIT limekuwa likitoa fedha za ufadhili sio chini ya Sh. 1.4 Bilioni kila mwaka
kwa Makanisa 10 ya Klasta ya Manyoni na kwa miaka 15 Makanisa yamepokea
takribani Sh. 18 Bilioni kwa ajili ya kuwahudumia watoto na vijana.
Alisema lengo la shirika hilo ni
kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia
Suluhu Hassan kwa kuwawezesha vijana kiuchumi na kutatua changamoto ya ajira.
Afisa Vijana Mkoa wa Singida Frederick Ndahani pamoja na kumshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuzindua mradi wa vijana hao na kuwakabidhi vitendea kazi mbalimbali vikiwemo pikipiki na mizinga vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh. 80.4 Bilioni amezishukuru Taasisi za dini kwa kuwajali na kuwasaidia vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa.
Dkt Mahenge akimkabidhi Kadi ya Bima ya Afya iCHF iliyoboreshwa Mzee Godwin Nguluga mara baada ya ufunguzi wa Zahanati ya Kijiji cha Maweni wilayani Manyoni katika Hafla iliyofanyika kijijini hapo jana wakati wa zaira yake ya kukagua miradi ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment