Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) Dk. John Jingu (aliyevaa miwani) akikabidhi bidhaa na chakula kwa viongozi na watoto wa Kituo cha Kulelea Watoto wenye Ulemavu Siuyu, Halmashauri ya Ikungi, mkoani Singida.
KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) Dk. John Jingu, amewataka wazazi wanaoishi na watoto wenye changamoto za ulemavu wa aina mbalimbali kuwathamini sanjari na kuwapa matunzo stahiki katika malezi na makuzi yao.
Jingu
aliyasema hayo alipotembelea na kutoa zawadi za bidhaa mbalimbali na chakula
kwa watoto wa Kituo cha Walemavu Siuyu, Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, mkoani
hapa leo.
“Wazazi
wawathamini watoto bila kujali hali zao. Kuna baadhi wanawaleta watoto kwenye
vituo na kisha kuwatelekeza…hii haikubaliki ni lazima tuzingatie haki za msingi
za malezi na makuzi ya watoto hususani watoto hawa wenye ulemavu,” alisema
Jingu
Aidha,
aliwataka Maafisa Ustawi wa Jamii nchini kuongeza kasi ya kuhakikisha
wanawatangamanisha watoto na wazazi wao-sambamba na jamii katika muktadha wa
kubadili fikra, mtazamo ili kuleta ustawi wa watoto hususan wale wenye aina
mbalimbali za ulemavu katika ngazi zote bila kubagua.
Kwa
mujibu wa Katibu Mkuu, kituo hicho cha Siuyu ni miongoni mwa vituo vyenye sifa
stahiki za utoaji wa huduma za malezi kwa watoto, ikiwemo usalama wa kutosha sambamba
na walimu waliosomea elimu maalumu ya watoto wenye ulemavu, huku akiwataka
viongozi wa vituo vingine nchini kuzingatia matakwa ya kisheria katika
uendeshaji wa huduma za usajili wa vituo vyao
“Moja
ya majukumu yetu ni kuvisajili na kuhakikisha vituo hivi vinafanya kazi
sawasawa. Hivyo nimekuja hapa kutembelea kituo hiki kwa lengo la kukagua lakini
nimeona pia nitoe zawadi kwa watoto hawa ambazo ni bidhaa na chakula,” alisema
Jingu
Hata
hivyo, Diwani wa Kata hiyo, Selestine Yunde, alimshukuru Katibu Mkuu kwa
kutembelea kituo hicho huku akimsihi kuangalia namna ya uwezekano wa serikali
kuanza kutenga bajeti za kuhudumia vituo hivyo.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Kituo hicho, Padre Tom Ryan, alisema ziara ya
viongozi wa serikali akiwamo Jingu hutafsiri faraja, ustawi na kuchagiza ustawi
na furaha kwa watoto hawa. “Tunaona fahari kwa kutiwa moyo na hamasa kupitia
zawadi hizi,” alisema.
Huku
mmoja wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho, Raymond Daudi, mbali ya
kushukuru, aliomba mamlaka ndani ya serikali kuangalia uwezekano wa kuwasaidia
watu wenye ulemavu, hususan wahitimu wa darasa la saba kwa kuwatengenezea
mazingira ya kujipatia kipato badala ya kuwaacha bila ya msaada wowote.
Awali,
akisoma taarifa ya kituo hicho, Kaimu Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida,
Paul Sangalali, alisema kituo hicho cha Siuyu, kilichopo wilaya ya Ikungi
mkoani hapa kilijengwa kwa ufadhili wa watu wa Ulaya na Marekani na
kilifunguliwa Februari 2007 na aliyekuwa Mhashamu Askofu wa Jimbo Katoliki
Singida, Desderis Rwoma.
Hata
hivyo, Sangalali alisema mbali ya mafanikio yaliyopo, kituo kinakabiliwa na
changamoto kadhaa zikiwemo uhitaji wa baiskeli kwa ajili ya watoto wenye
ulemavu wa viungo, uhitaji wa chakula, sabuni, mashuka na fedha kwa ajili ya
nauli ya kuwarudisha watoto nyumbani wakati wa likizo.
“Pia
miundombinu yake sio rafiki sana hasa pale watoto wanapokuwa wakielekea shule
ya msingi Siuyu, na kuna ushirikiano hafifu kwa wazazi kuchangia shilingi laki
moja za huduma kwa kila mwaka…lakini watoto wanapokuwa likizo nyumbani hawapati
mazoezi kwa wazazi hivyo wakirudi kituoni walimu hulazimika kuanza upya
kufundisha,” alisema Sangalali.
Katibu
Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya
Maendeleo ya Jamii) Dk. John Jingu (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi wa kituo
hicho Padre Tom Ryan, muda mfupi baada ya kukabidhi bidhaa na chakula kwa
viongozi na watoto wa Kituo cha Kulelea Watoto wenye Ulemavu Siuyu mkoani
Singida.
Mwonekano wa moja ya Jengo la huduma ndani ya kituo hicho
No comments:
Post a Comment