Ikungi - Singida
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe, Dk. Rehema Nchimbi amezindua miongoni mwa miradi mikubwa iliyowahi kutekelezwa nchini, mradi wa pamoja baina ya Mashirika ya Kimataifa ya UN Women na UNFPA kupitia ufadhiri wa Shirika la KOICA wa “Tuufikie usawa wa jinsia kupitia kuwawezesha wanawake na wasichana” utakaogharimu takribani bilioni 11.5 za kitanzania ambao utatekelezwa katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida na Msalala mkoani Shinyanga katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa.
Dk. Nchimbi amesema lengo kuu la mradi huo ni
kuchangia katika kuwawezesha wanawake na wasichana kuwakwamua kiuchumi na kijamii katika mikoa
ya Singida na Shinyanga ili kufikia
usawa wa kijinsia ambapo amewataka watendaji wote wa Serikali ambao
watatekeleza mradi huo kuwa makini katika utekelezaji wa mradi ili malengo ya mradi huo yaweze kufikiwa.
Amesisitiza kuwa Serikali
haitasita kuwachukulia hatua kali watendaji ambao kwa namna moja au nyingine hawataendana na
kasi ya utekelezaji wa miradi chini ya Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli
ambapo amesema mrai huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama
cha Mapinduzi ili kuwaletea
wananchi maendeleo ya kweli.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa
KOICA Tanzania, Bi Jieun Mo, walengwa wasio wa moja kwa moja
takribani wakazi 40,000 kutoka kwenye
wilaya ya Ikungi na Msalala na
walengwa wa moja kwa moja 2350 wanawake na wasichana kutoka katika wilaya hizo watanufaika na
mradi huu ambapo pia wanaume na wanawake
6000 wa Wilaya ya Ikungi watanufaika
kwenye eneo la muingiliano wa hati za
ardhi.
Mo ameainisha kuwa shughuli za mradi katika kuwaweza
wanawake kwenye eneo la uchumi
zitajikiza zaidi kwenye kuimarisha uwezo wa wanawake na vijana
wakulima ili waweze kutumia njia
nzuri za kilimo na hali ya hewa katika uzalishaji wa alizeti na kilimo cha
bustani, kukuza uuzaji wa pamoja, ujuzi wa ujasiriamali na wakala wa
uchumi wa wanawake na kuimarisha
usalama wa ardhi na umiliki.
Amesisiza kuwa shughuli hizo zitatekelezeka kupitia kuunda vikundi vya uzalishaji wa kilimo cha bustani
kwa wanawake, kuunganisha wanunuzi wa
vikundi vya wakulima vya
wanawake,kusaidia ujenzi wa ghala
kubwa moja la alizeti na kituo cha
ukusanyaji kilomo cha bustani ili
kuboresha uuzaji wa pamoja na utunzaji baada ya kuvuna, kutoa mafunzo ya
ujasiriamali, kutoa mafunzo ya ujasiriamali na ufikiaji wa habari za kifedha na
kufuatilia ushauri wa usimamizi wa biashara na
fedha na kukuza umiliki wa ardhi
pekee na wa pamoja wa wanawake kupitia
utoaji wa Hati za Haki za kimila za
Makaazi(CCROs).
Mwakilishi wa UN Women Bi, Hodan Addou ameishukuru Serikali ya
Tanzania kuwa ushirikiano wake
katika kuhakikisha kuwa mradi huu hatimaye umeanza kutekelezwa ambapo amesema
Shirika lake linaunga mkono juhudi za
Serikali za kumkomboa mwanamke ili kuondokana na unyanyasaji wa kijinsia.
Bi Addou amesisitiza kuwa
mradi utasaidia uwezeshaji kijamii kwa kuwawezesha wanawake kusimamia haki zao, kujenga ujuzi wa
ujasiiamali wa wanawake na wasichana kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia na kuimarisha
mifumo ya kuzuia na kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia kupitia kuanzisha na
kuandaa vifaa katika madawati matatu ya
Polisi ya Jinsia na Watoto, kuanzisha
vituo vitatu vya huduma ya dharura katika vituo vya wilaya, kuunda nafasi salama ya
umma, kujenga uwezo wa nambari ya msaada
ya watoto kitaifa, kuunda na kuimarisha Klabu za Wasichana na kuunda Kamati za
ulinzi na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Kwa upande wake Mwakilishi
Mkazi wa Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania Zlatan Milisic ameipongeza Serikali kwa kuwa na mradi huo na kuongeza kuwa mradi huo
unaendana na malengo ya endelevu ya 2030 hususani lengo namba 5 kuhusiana
kuwaendeleza wanawake katika nyanja
mbalimbali na kuongeza kuwa mwaka 2020 ni mwaka muhimu sana kwa kuwa
tunaelekea katika kutimiza miaka 25 ya
azimio la wanawake la Beijing.
Ameeleza kuwa malengo endelevu ya 2030 yameeleza kuwa ili
kufikia maendeleo ya nchi kumtambua mwanamke ni jitihada muhimu sana katika kuharakisha na kutimiza malengo yote
ya maendeleo ambapo ameihakikishia Serikali ya Tanzania kuendelea kufanya kazi
kwa karibu sana ili kuhakikisha wanawake
wanakuwa chachu ya maendeleo katika nchi
ya Tanzania.
Mwakilishi wa UNFPA, Dk.
Winfred amesema kuwa uzinduzi wa mradi umelenga kutokomeza aina zote za
unyanyasaji wa kijinsia na kuimarisha
usawa katika jamii ikiwa ni pamoja na
kuimarisha maisha ya wanawake ambapo amesisitiza kitovu cha matatizo ya
kijinsia ni wanaume na mila na desturi
potofu zinazomtazama mwanamke kwa kumdharirisha hivyo juhudi za makusudi zinatakiwa
kufanywa za kuwaweka wanaume mbele ili kutokomeza unyanyasaji wa
kijinsia kwa wanawake.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Edward Mpogolo amesisitiza kuwa kazi nzuri zinazofanywa
na Rais John Pombe Magufuli katika
Nyanja mbalimbali ndiyo zinazoyafanya
jumuiya za kimataifa kuunga mkono
kwa kutoa misaada kupitia miradi mbalimbali hapa nchini.
No comments:
Post a Comment