Sunday, April 28, 2019

KATIBU TAWALA MKOA WA SINGIDA DKT. ANGELINA LUTAMBI, AMEONGOZA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA MWANAMKE WA NGUVU 2019, MKOANI SINGIDA.


Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi ameongoza maelfu ya wanawake waliohudhuria na wengine kufuatilia kupitia redio standard (90.1 fm) mkoani Singida katika kuadhimisha kilele cha Siku ya Mwanamke wa Nguvu 2019 mkoani Singida huku akiwataka Wanawake kujiunga katika vikundi vya wajasiriamali ili kupata fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali pamoja na taasisi zisizo za kiserikali.

Dkt. Lutambi amesema, mwanamke anapojiunga katika kikundi cha wajasiriamali itasaidia hata kwa familia kuwa imara kiuchumi. Mwanamke anapojituma katika kufanya shughuli mbalimbali za kuingiza kipato manufaa yanayopatikana ni kwa wote ndani ya familia (baba, mama na watoto).

Akitaja baadhi ya fursa amesema, yapo manufaa mengi ndani ya kikundi cha wajasiriamali ambapo mwanakikundi atanufaika na mikopo isiyo na riba inayotolewa na Serikali, elimu ya biashara (ujasiriamali), mbinu mbalimbali za kuongeza thamani za bidhaa sambamba na kutafutiwa masoko ya ndani na nje ya nchi ili kuinua uchumi wa familia na Taifa.

“Sisi wanawake tunayo majukumu mengi sana katika familia. Familia ambayo mama hajitambui ni familia ambayo inakosa msingi, ni familia ambayo inakosa nguvu, lakini sisi tumethubutu.”

“Ndugu zangu wakinamama wa Singida, uwepo wetu katika jamii unamchango mkubwa sana, vikundi tunavyovianzisha vinatufanya tusimame,
tunafahamu kwamba wapo ambao wenyeuwezo wa kusimama wenyewe lakini wengi wetu hatuwezi, tunahitaji kukusanyana na kushikana kwa pamoja ili  kuongeza nguvu, kwa umoja wetu tunaweza kusimama na kushinda changamoto zote zinazoweza zikatukabili”. Dkt. Lutambi.

 “Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, anatuambia HAPA KAZI TUU, kila mtu afanye kazi. 
Kauli hiyo siyo maneno tuu bali anamaanisha; kauli hiyo anatuambia sisi wanawake tuamke, sisi wanawake tulionguzo katika familia zetu tusimame imara, tujishughulishe, na tukifanya hivyo tutakuwa tumelibeba taifa letu na kulisogeza pale linapotakiwa kuwa.

Akifafanua zaidi, Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Lutambi amesema, kumuinua mwanamke kiuchumi ni kuinua Taifa, kwa sababu mwanamke anauwezo wa kusimama na kusimamia yale anayoyaamini. Mwanamke anapofanya kazi ya kuingiza kipato italifanya taifa lionekane ni taifa kati ya mataifa na kulisogeza kiuchumi.

Katika kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa, Dkt. Lutambi amewahimiza wanawake mkoani Singida kujitokeza kwa wingi katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi yoyote bila kusita kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

“Mwanamke wa nguvu usibaki nyuma, lazima ugombee katika ngazi yoyote ile ili kuleta maendeleo katika maeneo ulipo” Dkt. Lutambi.

Pia, amewasisitiza wanawake kujiunga na mfuko wa afya ya jamii ulioboreshwa (iCHF) ambapo kwa gharama ya shilingi elfu thelasini itahudumia kaya moja (baba, mama na watoto 4 kwa mwaka). Faida za mfuko huo ni kupata huduma za matibabu katika hospitali zote zilizounganishwa na huduma hiyo mahali popote pale ndani ya mkoa, iwe kituo cha afya, hospitali ya wilaya au hospitali ya Rufaa.

“Kwa kawaida ugonjwa haubishi hodi, hivyo niwaombe wanawake wenzangu, ni vyema kujiunga na mfuko wa bima ya afya ulioboreshwa ili kuzilinda familia zetu kiafya na kufanya familia kuwa bora zaidi. Na haya yote ni manufaa ya Serikali yetu katika kumsaidia mwanamke”. Dkt. Lutambi.

Aidha amewapongeza wanawake wote waliojitokeza na kujiunga katika vikundi mbalimbali vya wajasiriamali ili kujishughulisha kwa ajili ya familia zao, kwa ajili ya mkoa na taifa ambapo amesema jambo hilo ni mchango mkubwa sana kwa jamii inayotuzunguka kwani mwanamke ni nguvu na ni nguzo katika familia na kwa maendeleo ya taifa.

Dkt. Lutambi amewasisitiza wanawake hao kufanya kazi kwa bidii sambamba na kuwa na vitambulisho vya wajasiriamali na amewahakikishia kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano ipo bega kwa bega na wajasiriamali katika kuhakikisha wanavushwa kutokana na changamoto mbalimbali walizonazo ili kufikia uchumi wa kati.

Naye, mkurugenzi wa radio standard Fm ya mkoani Singida Bw. James Daudi, amewahimiza wanawake kujituma katika kufanya kazi huku akisema pesa haimjui mtu bali pesa inamjua mtu anayeitafuta. Hivyo ni lazima mwanamke kujituma, kujiunga katika vikundi vya wajasiriamali ili kuibua hamasa kwa kuhamasisha mwanamke kuweza kujitegemea.

“Pesa iko juu mlimani, anayetengeneza kama vile ni maji yapo juu, unachotakiwa ni kutengeneza mfereji, usipotengeneza mfereji maji yanakwenda kwa mwenzako aliyetengeneza mfereji. Dunia nzima imejaa pesa nyingi mno lakini zinakuja kwa yule mtu aliyezitengenezea mfereji". Bw. Daudi.

Amesema, wapo wakinamama wanaoshinda kwenye vioo na vipodozi tuu huku wakilalamika juu ya ugumu wa maisha badala ya kufanya kazi kwa kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali yetu kupitia vikundi vya wajasiriamali zikiwemo ushonaji, vikundi vya wafugaji, kilimo na biashara.

Akiendelea kuzungumza na wanawake wajasiriamali hao, Mkurugenzi huyo amewaambia wanawake kuwa na desturi ya kusikiliza redio ili kupata taarifa mbalimbali juu ya mambo mazuri yanayofanywa na Serikali zikiwemo fursa mbalimbali, na kusema mwanamke anaweza kuwa anavyotaka mwenyewe.

Naye, Afisa Maendeleo ya Jamii, Dawati la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Manispaa ya Singida Bw. Tumaini Christopher, akizungumzia umuhimu wa Wanawake kushiriki fursa za Maendeleo amesema, maendeleo endelevu na jumuishi yanasisitiza ushiriki wa jamii katika kupanga, kuamua, kutekeleza, kusimamia na kutathimini.

Amesema, wataalam wa Maendeleo ya jamii wanazo stadi za kutumia mbinu shirikishi zinazowezesha kuamsha ari ya jamii kushiriki katika maendeleo yao ikihusisha watu wote na makundi mbalimbali katika jamii. Stadi hizo ni pamoja na kuelimisha, kuhamasisha na kuraghibisha jamii katika kujiletea maendeleo.

Akizungumzia usawa wa Kijinsia Bw. Christopher amesema .
"Tanzania imefanikiwa kufikia asilimia 37 ya wanawake Bungeni, asilimia 41 wanawake Majaji na asilimia 30 wanawake Madiwani"

"Kutokana na jitihada hizo za Serikali, wanawake wanaendelea kuaminika na kuchukua nafasi za juu za uongozi na maamuzi ikiwemo nafasi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais na Naibu Spika". 

Kwa upande wao, wanawake hao wa nguvu 2019 mkoani Singida wameishukuru Serikali kwa fursa mbalimbali za maendeleo zinazotolewa kwa ajili ya kumuinua mwanamke kielimu, kisiasa na kiuchumi.

Sherehe hizo zilihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa shirika la SIDO mkoani Singida, pamoja na wajumbe mbalimbali kutoka kwa wadhamini NHIF, MAASA SCHOOL, IR VIKOBA na benki ya NBC mkoani Singida.

MATUKIO KATIKA PICHA 





Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi akikata keki iliyotengenezwa na wanawake wajasiriamali ili kuashiria kuunga mkono kazi zinazofanywa na wanawake hao, wakati akitembelea mabanda mbalimbali ili kujionea ubunifu unaofanywa na wajasiriamali hao wakati wa kilele cha maadhimisho wa siku ya Mwanamke wa Nguvu 2019 mkoani Singida.
   
 SEHEMU YA MEZA KUU 
katika siku ya kilele cha maadhimisho wa Mwanamke wa Nguvu 2019 mkoani Singida.


Mratibu IR Vikoba mkoani Singida, Bi. Happy Francis akitoa wito kwa wanawake kujiunga na vikundi ili kupata ujuzi, mikopo, na taarifa mbalimbali za maendeleo kwa mwanamke kiuchumi.

Bi. Happy Francis, anajishughulisha na ufugaji wa kuku aina ya Kroiler na Sasso pamoja na usindikaji wa vyakula katika manispaa ya Singida mkoani Singida.



Wajasiriamali mbalimbali wakizungumza, wakati wa kilele cha maadhimisho wa siku ya Mwanamke wa Nguvu 2019 mkoani Singida.

 Meneja wa SIDO mkoa wa Singida akizungumza na wajasiriamali wanawake, wakati wa kilele cha maadhimisho wa siku ya Mwanamke wa Nguvu 2019 mkoani Singida.

Mkuu wa chuo cha ufundi kwa watu wenye ulemavu cha Sabasaba Manispaa ya Singida Bi. Fatuma Malenga, akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Mwanamke wa Nguvu 2019 mkoani Singida. Aidha amewataka  wanawake na jamii kwa ujumla kuwaleta chuoni watu wenye ulemavu ili kujipatia elimu ya ufundi stadi; Ushonaji, kilimo cha kisasa, umeme na kazi zingine za mikono kama kutengeneza sabuni n.k. Pia watafundishwa namna bora ya kuwa wajasiriamali.

"Wanawake wenye ulemavu nao pia wanastahili kuwa wanawake wa nguvu, tuhakikishe hakuna anayeachwa nyuma." Amesema Malenga.

Afisa Maendeleo ya Jamii, Dawati la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Manispaa ya Singida Bw. Tumaini Christopher, akizungumza, wakati wa kilele cha maadhimisho wa siku ya Mwanamke wa Nguvu 2019 mkoani Singida.

Mkurugenzi wa radio standard Fm ya mkoani Singida Bw. James Daudi (kulia) akizungumza, wakati wa kilele cha maadhimisho wa siku ya Mwanamke wa Nguvu 2019 mkoani Singida.

Baadhi ya wanawake waliojitokeza kuadhimisha kilele cha maadhimisho wa siku ya Mwanamke wa Nguvu 2019 mkoani Singida.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi akikabidhi tuzo ya mhamasishaji na mwanaharakati, Mratibu IR Vikoba mkoani Singida, Bi. Happy Franciswakati wa kilele cha maadhimisho wa siku ya Mwanamke wa Nguvu 2019 mkoani Singida.


Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi akikabidhi tuzo ya ujasiriamali kwa mbunifu wa mavazi (nguo za kufuma), Bi. Annastazia Masanja kutoka kikundi cha Faraja Group cha Utemini manispaa ya Singida, wakati wa kilele cha maadhimisho wa siku ya Mwanamke wa Nguvu 2019 mkoani Singida.




Wajasiriamali wa ubunifu wa mavazi (nguo za kufuma), kutoka kikundi cha Faraja Group cha Utemini manispaa ya Singida, wakati wa kilele cha maadhimisho wa siku ya Mwanamke wa Nguvu 2019 mkoani Singida.



Picha ya pamoja meza kuu pamoja na wajasiriamali mbalimbali, wakati wa kilele cha maadhimisho wa siku ya Mwanamke wa Nguvu 2019 mkoani Singida.

Picha ya pamoja meza kuu pamoja na wasichana wenye ulemavu, wakati wa kilele cha maadhimisho wa siku ya Mwanamke wa Nguvu 2019 mkoani Singida.

Picha ya pamoja meza kuu pamoja na wafanyakazi wa redio standard ya mkoani Singida, wakati wa kilele cha maadhimisho wa siku ya Mwanamke wa Nguvu 2019 mkoani Singida. 

IMETOLEWA NA;
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO
OFISI YA MKUU WA MKOA
SINGIDA

No comments:

Post a Comment