BAADA ya Rais Dkt. John Magufuli kurejesha Kikokotoo cha zamani kwa
mafao ya WATUMISHI WA UMMA nchini, wafanyakazi kupitia mashirikisho huru ya
vyama wameendelea kuunga mkono agizo hilo kwa kufanya maandamano ya
amani.
Shirikisho
huru la vyama vya wafanyakazi Mkoa wa Singida, leo limefanya maandamano ya
amani ya kumpongeza Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kwa kuondoa tatizo la
KIKOKOTOO ambacho kilisababisha watumishi wengi kukosa amani na utulivu mioyoni
mwao.
Maandamano
hayo yaliyoanzia ofisi za TUCTA mkoa zilizopo mtaa wa Mughanga na kupitia mtaa wa
Boma road kisha kupokelewa katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Singida na Dkt.
Rehema Nchimbi ambaye ndiye mkuu wa mkoa wa Singida akisindikizwa na viongozi mbalimbali wa Vyama na Serikali.
Katika
risala ya watumishi hao iliyosomwa na Katibu wa TUCTA mkoa, Bw. Max Chaba,
wafanyakazi hao wamepongeza hatua ya Mheshimiwa Rais Magufuli kurejesha
kikokotoo cha zamani, hali waliyoieleza kuwa amesikiliza maombi yao na sasa
amefuta machozi yaliyokuwa yakiwatoka kwa muda mrefu sana.
Katibu
huyo wa TUCTA amesema kuwa, uamuzi wa Rais Magufuli umepokelewa kwa furaha sana na
watumishi wote wa mkoa wa Singida na Tanzania kwa ujumla.
“Uamuzi huu umerejesha hali
na morali ya watumishi wa umma nchini katika kufanya kazi kwa nguvu zao zote. Hii
inatokana na imani kwamba baada ya kustaafu kuna kitu ambacho watakipata chenye
nafuu cha kumwezesha kujikimu yeye mwenyewe na familia yake” Bw. Max amesema.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa TUCTA mkoa wa Singida, Bw. Emmanuel Misholi, amesema
kikokotoo kilichotangazwa awali kilikuwa ni JENEZA lililoandaliwa kwa ajili ya
watumishi wanaotarajiwa kustaafu.
“Kwa
kweli Rais Magufuli ni kiongozi msikivu mno amesikia kilio chetu na kuchukua
hatua stahiki. Binafsi nina furaha na amani moyoni haijawahi kutokea. Sisi kama
watumishi wa umma, hatuna zawadi ya kumpa Dkt. Magufuli isipokuwa ni kuchapa
kazi na kukidhi mahitaji ya Watanzania wote bila ubaguzi” amesema Misholi.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amempongeza Rais kwa
uamuzi wa busara, huku akiwataka watumishi wa mkoa wa Singida kuendelea kumuunga mkono
Mheshimiwa Rais Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii zaidi ili kuleta ufanisi.
Mkuu
huyo wa mkoa wa Singida, amewataka watumishi wa umma mkoani hapa kutumia furaha
yao na amani waliyoipata baada ya kikokotoo kufutwa, kuongeza bidii ya kazi mara dufu katika kuitumikia
Serikali na Watanzania ikiwa ni kumshukuru Rais Magufuli kwa kusikia kilio
chao hicho cha muda mrefu.
Aidha,
Dkt. Nchimbi amewaagiza wakuu wote wa idara, vitengo na viongozi wengine mkoani Singida,
waendelea kuwa karibu na watumishi walio chini yao, na tabia ya kukemea,
kuwatishia, isiwepo ili kumfanya mfanyakazi kuwa na amani wakati wote awapo
kazini.
“Wafanyakazi, jambo hili ambalo mmelitambua na kuja
kulisherekea leo kwa maandamano ya amani kwa ajili ya kumpongeza na kulitolea
shukrani kwa Mheshimiwa Rais Magufuli ni jambo kubwa sana kwa uhai na uhai endelevu
wa utumishi wetu na matunda ya kazi zetu”
“Hakika hakukukuwa na namna nyingine yoyote ya kusema
isipokuwa ni kutoka na kusema hongera mheshimiwa Rais asante sana kwa haya yote
uliyotufanyia na hasa la kutuondolea tatizo hili la kikokotoo… hongera mheshimiwa
Rais Magufuli”.
“Waheshimiwa sana wafanyakazi, mnahaki tena mnahaki sana ya
kumpongeza Rais na hata mngeamua kushinda kutwa nzima hapa kwa kumpongeza Rais mnahaki, na
msiishie hapa endeleeni kumpongeza popote pale, hata mkiwa kwenye madawati yenu endeleeni
kumpongeza. Hili la kikokotoo hili, sio letu ni la familia zetu na taifa kwa
ujumla” amesema Dkt. Nchimbi kwa furaha tele.
Awali
akizungumza baada ya kupokelewa maandamano, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida,
Bw. Juma Kilimba, aliwaomba watumishi wa umma kufanya kazi karibu zaidi na
Serikali yao ili kuunga mkono utekelezaji wa sera za Chama Cha Mapinduzi.
Kanuni
ya kikokotoo kipya kilichokuwa kinalipa asilimia 25 ya mafao ya watumishi,
kililalamikiwa sana na kupingwa na wadau wengi nchini, hali iliyomlazimu Rais
Magufuli kuingilia kati na kurejesha utaratibu wa zamani.
Maandamano
haya yameaandaliwa na chama cha wafanyakazi TUCTA mkoa wa Singida kwa
ushirikiano na vyama vya CWT, TUICO, TALGWU, TUGHE, RAAWU pamoja na TAMICO kwa lengo
la kumshukuru na kumpongeza Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa kufuta kikokotoo.
"Mheshimiwa Rais John Magufuli Oyeeee"!!!
Oyeeeeeeeee!!!" Ndivyo sauti za shangwe na vifijo vilivyokuwa vikitawala kwenye sherehe hizi za pongezi kwa Rais kutoka kwa waandamanaji hao.
MATUKIO KATIKA PICHA
'Solidarity Forever' Mshikamano Daima'
IMETOLEWA NA;
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO,
OFISI YA MKUU WA MKOA
SINGIDA
No comments:
Post a Comment