Viongozi wa Kamati
ya Dini mbalimbali mkoa wa Singida wamewatakia Heri na Baraka wananchi wote wa mkoa
wa Singida na Tanzania kwa ujumla katika kipindi hiki cha Krisimasi na kuelekea
mwaka mpya 2019, na kuwataka wananchi kusherekea kwa amani na utulivu.
Salamu hizo
zimetolewa leo na viongozi hao walipokutana katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt. Rehema Nchimbi na wameahidi kuendeleza maombi kwa nguvu zote kwa
ajili ya kumuombea Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Magufuli na Tanzania, ili
iendelee kuwa kisiwa cha amani na utulivu.
Makamo mwenyekiti Askofu
Kaale akisoma taarifa “Mwanadamu anapoishi hapa duniani hawezi akapata
amani kutokana na vitu alivyonavyo kwa wingi kama fedha, dhahabu, magari,
nyumba, mashamba na viwanja. Kwa sababu hiyo amani ya Mungu hupatikana kwa
Mungu peke yake”
“Tunawahamasisha Watanzania na Singida yetu kwamba kila mtu ampe
nafasi Mungu wa kweli amtawale ili kusababisha Amani ya kweli katika nchi yetu
ya Tanzania”
Imedaiwa kuwa, amani
na utulivu iliyopo nchini Tanzania, imechangia kwa kiasi kikubwa kwa Mheshimiwa
Rais wa awamu ya TANO, Dkt. John Magufuli kuishangaza dunia kwa juhudi zake za
kuanzisha miradi mikubwa ya maendeleo ndani ya miaka mitatu.
Katika kuijengea
nguvu hoja yao hiyo, Askofu Kaale, alinukuu Maandiko Matakatifu kutoka katika Biblia
kitabu cha Isaya 32:17 inayosema “Na kazi ya haki itakuwa amani; na mazao ya haki yatakuwa utulivu na
matumaini daima”.
“Sisi Kamati ya Dini mbalimbali hapa Mkoa wa Singida, tunaziona
na kuzipongeza jitihada za Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Dkt. John Joseph Magufuli”
“Ipo miradi mingi iliyotekelezwa na Serikali ndani ya miaka
mitatu ya Rais Magufuli. Amesimamia misingi ya Uchumi, pamoja na changamoto
kadhaa zinazoikumba uchumi wa dunia na hata ukanda wa Afrika, Kusini mwa Jangwa
la Sahara”
“Katika mwaka 2017/2018 uchumi wa Tanzania umekuwa kwa asilimia
7.1 na kuifanya kuwa ya kwanza kwa Afrika Mashariki, lakini katika takwimu
zilizotolewa na Benki ya Dunia (WB) ni ya Tisa kati ya nchi 10 duniani ambazo
uchumi wake unakuwa kwa kasi zaidi” Askofu Kaale akisoma taarifa.
Aidha, Viongozi
hao kutoka Madhehebu mbalimbali ya mkoa wa Singida wamesema kwa umoja wao,
wanaiunga mkoa Serikali ya Awamu ya Tano na kuwaasa watanzania kuendeleza
utamaduni wa kulipa kodi ili fedha hizo zitumike kukamilisha miradi ya
maendeleo katika taifa letu la Tanzania.
Naye kiongozi wa
dhehebu la Kiislamu mjini hapa, Mbiaji Hassan, ametumia fursa hiyo kuyaomba
madhehebu mengine yasiwe kikwazo kwa sikukuu hii ya Krismasi na kuelekea mwaka mpya 2019
na ameyasihi kuhakikisha sikukuu hizi zinasherekewa kwa amani na utulivu.
Hafla hiyo
imehudhuliwa na mkuu wa mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi pamoja na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, ACP
Sweetbert Njewike.
Kwaupande wake, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, ACP,
Njwewike, amewatoa hofu waumini wa madhehebu ya dini ya Kikristo na mengine na kwamba
wamejipanga vema kuhakikisha sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya zinapita vizuri
bila kikwazo au usumbufu wa aina yoyote mkoani Singida.
Naye, Mkuu wa mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi, amesema ni
ukweli usiopingika kwamba bei ya amani ni ndogo mno, lakini ikitoweka gharama
yake ya kuirejesha ni kubwa mno.
“Kutokana na ukweli huo, natarajia kila mkazi wa mkoa huu
uliopo jirani na makao makuu ya nchi anashiriki kuitunza na kuilinda
amani na utulivu kama ilivyo kwa utamaduni wa mkoa wa Singida. Krismasi haipo
kwa ajili ya kumuudhi mtu, ipo kwa ajili ya sherehe zinazotawaliwa na amani”, amesema
Dkt. Nchimbi.
Hata hivyo, ametoa
wito kwa familia kutumia sikukuu hizi kwa kukaa na familia zao ili kusherekea
kwa amani na umoja na amesisitiza kwa wazazi kuwa waangalifu kwa watoto wao.
“Kipindi hiki cha
mwisho wa Mwaka ndicho ambacho familia zinatakiwa zikae na kutafakari mwaka
mzima yote ambayo yamefanyika na ambayo tumekutana nayo, wapi tumekwenda vizuri,
wapi hatukufanikiwa sana. Familia zikae pamoja zitafakari kwa pamoja na katika
umoja wetu ni lazima tutashinda”
“Na unapokuta
viongozi wa dini mbalimbali wanakaa pamoja na wanakuwa na nia moja na
wanawafikia wananchi wao ambao ni waamini wao kwa pamoja, kwa vyovyote mahali
hapo Mungu yupo”, Dkt. Nchimbi akielezea zaidi.
“Singida yetu ni
Singida ya umoja, ni Singida ya upendo, ni Singida ya mshikamano, ni Singida ya
amani, ni Singida ya utulivu na ni Singida ya maendeleo”
“Wakati huu wa Sikukuu
ya Noel na mwaka mpya 2019, nawatakia Watanzania wote moyo wa Upendo, Furaha,
Ukarimu na Amani kwa kila mtu,
Salamu kuu: “Dini Mbalimbali - Upendo na Amani"...
MATUKIO KATIKA PICHA
Mwenyekiti wa Kamati ya dini mbalimba mkoa wa Singida Alhaj. Hamis Kisuke akizungumza.
Mkuu wa mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi (kushoto) pamoja na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, ACP Sweetbert Njewike wakisikiliza kwa makini na kupokea salamu za sikukuu za Krismasi na mwaka mpya 2019 kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Singida kutoka kwa Kamati ya Dini mbalimbali mkoa wa Singida.
Kiongozi wa dhehebu la Kiislamu mjini Singida, Mbiaji Hassan akizungumza.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, ACP Sweetbert Njewike akizungumza.
Viongozi wa Kamati ya Dini mbalimbali mkoa wa Singida wakikabidhi kwa maandishi Salamu za Krismasi na Mwaka mpya 2019 kwa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi.
IMETOLEWA NA'
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO
OFISI YA MKUU WA MKOA
SINGIDA.
No comments:
Post a Comment