Friday, July 29, 2016

RAIS DKT JOHN POMBE MAGUFULI AWAONYA WANASIASA WANAOTAKA KUFANYA MAANDAMANO.












Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew Mtigumwe kushoto kwake ni Mama Janet Magufuli mara baada ya kuwasili Wilayani Manyoni Mkoani Singida.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaonya wanasiasa mbalimbali wanaotangaza kufanya maandamano kinyume cha sheria na kuvuruga amani ya nchini kuwa wasimjaribu.

Rais Magufuli ameyasema hayo mapema leo katika viwanja vya Shule ya Msingi Tambuka reli Wilayani Manyoni alipokuwa akihutubia mamia ya wakazi wa Mkoa wa Singida waliojitokeza kumpokea katika siku yake ya kwanza ya ziara ya kikazi Mkoani hapa.

Amesema kuwa wananchi wana matatizo na kero nyingi hivyo anataka kujikita katika kutatua kero hizo na sio kupoteza muda kuzuia maandamano yasiyofuata sheria huku akiwasihi wananchi kufanya kazi kwa bidii.

Aidha, Rais Magufuli amewaeleza wakazi wa Mkoa wa Singida kuwa serikali yake iko katika mpango wa kujenga madarasa na kukarabati shule za sekondari ikiwemo shule kongwe ya Mwenge iliyoko Manispaa ya Singida mara baada ya zoezi la kutengeneza madawati kukamilika.

Ameongeza kuwa wananchi wa Singida wanapaswa kuzalisha kwa wingi alizeti ili kukidhi mahitaji ya kiwanda kikubwa kilichopo Mkoani hapa, pia amewataka wafanyabiashara na wakulima wa zao la vitunguu kufungasha vizuri vitunguu hivyo ili wapate wanunuzi kutoka nje ya nchi.

Amesema serikali yake itahakikisha inakamilisha ujenzi wa barabara ya lami kutoka Manyoni hadi Tabora katika eneo dogo lililobaki, pia itajenga reli kutoka Dar es Salaam kupitia Manyoni hadi Rwanda na Burundi.

Rais Magufuli amesisitiza azma yake ya kuhamia Dodoma kuwa lazima itimie kwakuwa ilishapangwa hivyo tangu enzi za Hayati Julius K. Nyerere na yeye anatekeleza huku akiwataka wananchi wa Manyoni kuitumia fursa hiyo kuwekeza kwani watakuwa karibu na makao makuu ya nchi. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia mamia ya wakazi wa Manyoni Mkoani Singida mara baada ya kuwasili katika Wilaya hiyo.
 
Wananchi wa Manyoni wakishangilia Hotuba nzuri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa katika mkutano wa Hadhara kwenye Uwanja vya Shule ya Msingi Tambuka Reli Manyoni Mkoani Singida.

Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akiwasalimia wakazi wa Singida.

No comments:

Post a Comment