Saturday, July 30, 2016

RAIS MAGUFULI AKAMILISHA ZIARA MKOANI SINGIDA; AMUAGIZA MKANDARASI WA DARAJA LA SIBITI KURUDI 'SITE' MARA MOJA.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli akihutubia wakazi wa Wilaya ya Iramba katika uwanja wa Soko la Misigiri mapema asubuhi ya Leo.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John P. Magufuli amemuagiza Mkandarasi wa kampuni ya Hainan International Limited anayejenga daraja la Sibiti Mkoani Singida kuendelea na ujenzi wa daraja hilo la sivyo atateua Mkandarasi mwingine.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo asubuhi katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Iramba katika viwanja vya soko la Misigiri wilayani Iramba huku akisisitiza kuwa pesa ya kumlipa Mkandarasi huyo ipo tayari hivyo anatakiwa kuendelea na ujenzi haraka.

Amesema daraja la Sibiti lilioko Wilayani Mkalama linaunganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Simiyu ni muhimu kwa uchumi wa wananchi wa mikoa hiyo na kumtaka Meneja wa Barabara Mkoani Singida Mhandisi Leonard Kapongo kusimamia utekelezaji wa agizo hilo.

Aidha amewataka wananchi Mkoani Singida kuendeleza kufanya kazi kwa bidii, kiutunza amani ya nchi bila ubaguzi wowote huku akiwasisitiza watendaji wote wa serikali kuwahudumia wananchi kwa uadilifu mkubwa.

Rais Magufuli amezitaka halmashauri kutowanyanyasa wakulima wadogo wadogo kwa ushuru wa mazao kidogo wanayoyapata bali halmashauri zikusanye kodi kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa na vyanzo vingine halali.

Rais Magufuli amekamilisha ziara yake Mkoani Singida mapema leo asubuhi mara baada ya kufanya mikutano ya hadhara na wananchi wa Manyoni, Singida na Misigiri huku msafara wake ukisimamishwa na wananchi wa Ikungi. 
Wakazi wa Singida wakimsikiliza kwa makini Rais Magufuli katika viwanja vya people's club Mjini Singida

Mkatibu Tawala wasaidizi wa Sekretariet ya Mkoa wa Singida wakimsikiliza kwa makini Rais Magufuli katika uwanja wa soko la Misigiri.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dokta Angelina M. Lutambi (wa kwanza aliyevaa miwani) akimsikiliza kwa makini Rais Magufuli katika uwanja wa soko la Misigiri.

Wabunge wa Mkoa wa Singida wakiwa pamoja na Rais Magufuli wakati akihutubia katika uwanja wa soko la Misigiri.

No comments:

Post a Comment