Wednesday, August 03, 2016

MKUU WA MKOA AWAASA WALIMU MAHIRI KUINUA UBORA WA ELIMU MSINGI MKOANI SINGIDA.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe (picha ya maktaba).

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe amewaasa walimu mahiri 532 wa masomo ya hisabati, kiswahili na kiingereza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa ili kuinua ubora wa elimu Msingi Mkoani Singida.

Mhandisi Mtigumwe ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo  kwa walimu mahiri wa darasa la tatu na la nne juu ya uimarishaji stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu huku mafunzo hayo  yakifadhiliwa na mradi wa Literacy and Numeracy Education Support (LANES).

Amesema mafunzo hayo ni mwendelezo wa utekelezaji wa lengo la Serikali la kuimarisha na kuboresha elimu katika ufundishaji na ujifundishaji ngazi ya elimu msingi ili kuendana na maboresho ya ya mtaala wa darasa la kwanza  na la pili na sasa darasa la tatu na la nne.

Mhandisi Mtigumwe ameongeza kuwa mwisho wa mafunzo hayo walimu wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa kazi zao ikiwemo kutoa mrejesho kwa mazazi au mlezi kuhusiana na maendeleo ya mtoto huku wakizingatia maadili mema na utendaji kazi mzuri.

Naye Mratibu wa Mafunzo ngazi ya Mkoa ambaye ni afisa elimu taaluma Mkoa Eva Mosha amesema mafunzo hayo yatamjengea umahiri mwalimu katika ufundishaji na ujifunzaji, maandalizi ya ufundishaji na ujifunzaji wenye kuzingatia umahiri na uchopekaji wa kusoma, kuandika na kuhesabu katika darasa la tatu na la nne.

Mosha ameongeza kuwa walimu hao wataongezewa ujuzi juu ya matumizi  ya mbinu mbalimbali za ufundishaji na ujifunzishaji na utengenezaji wa zana mbalimbali zinazotumika katika ufundishaji wa masomo mbalimbali hasa masomo ya kusoma, kuandika na kuhesabu.

Mratibu wa Mafunzo ngazi ya Mkoa ambaye ni afisa elimu taaluma Mkoa Eva Mosha akizungumza na washiriki wa mafunzo.

Walimu wakipata mafunzo juu uimarishaji wa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.

No comments:

Post a Comment