Friday, August 05, 2016

ONGEZEKO LA WATOTO WANAOISHI KATIKA MAZINGIRA HATARISHI MKOANI SINGIDA;WADAU WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI.


Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida Shukrani Mbago akizindua rasmi kituo cha Amani cha  watoto wanaoishi Mtaani.

Wadau mbalimbali wa ulinzi na usalama wa mtoto wameombwa kushirikiana na serikali kupambana na tatizo la ongezeko la watoto wanaoshi katika mazingira hatarishi Mkoani Singida.

Afisa ustawi wa jamii Mkoa wa Singida Shukrani Mbago ametoa wito huo wakati akizindua kituo cha Amani ambacho kinajishughulisha na kuwatoa watoto wanaoishi mtaani na kuwarudisha kwa wazazi na walezi wao.

Mbago amesema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2014/2015 watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi Mkoani Singida ni 36,246 huku watoto wanaoishi mitaani wakifikia 2,697 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012.

Ameongeza kuwa Mkoa wa Singida una jumla ya vituo vinavyohudumia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi vitano na kusema kuwa  idadi hiyo ni ndogo kulingana na ukubwa wa tatizo huku akiwasihi wadau mbalimbali wajitokeze kuongeza vituo hivyo.

Mbago amesema kituo cha Amani ni kituo pekee Mkoani Singida ambacho kimejikita katika kuwasaidia watoto wanaoishi mitaani kwa kuwapa huduma za chakula, malazi, matibabu na kuwaunganisha watoto hao na familia zao.

Kwa upande wake Mratibu wa Kituo cha Amani Singida Editruda Kifumu amesema kituo hicho kina jumla ya watoto kumi huku mtoto mmoja akiwa tayari ameunganishwa na familia yake.

Kifumu amesema huduma za kituo cha Amani ziko wazi kwa watoto wote wa mtaani Singida na kuwasihi wadau na serikali kuendelea kutoa ushirikiano kwa kituo hicho.

Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida Shukrani Mbago (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watoto na walezi wa kituo cha Amani mara baada ya kukizindua kituo hicho.

No comments:

Post a Comment