Wednesday, August 10, 2016

SERIKALI YATOA AGIZO KWA WAZAZI NA WALEZI KUHUSU PESA ZA TASAF.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina M. Lutambi akizungumza na walengwa wa Tasaf kijiji cha Iguguno Wilayani Mkalama, kushoto kwakwe ni Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Singida Eva Mosha na kulia kwake ni Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Singida Patrick Kasango.



Serikali Mkoani Singida imewaagiza wazazi na walezi wanaopata ruzuku ya elimu kupitia mpango wa TASAF III  wafuatie kwa karibu maendeleo ya watoto wao shuleni  ili waje kuzikomboa kaya maskini kutoka lindi la umaskini.

Kufuatilia huko kuwe pamoja na kukagua madaftari ya wanafunzi mara kwa mara ili kujiridhisha na maendeleo ya mwanafunzi husika.

Agizo hilo limetolewa juzi na Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi wakati akizungumza muda mfupi kabla ya zoezi la kugawa fedha za ruzuku za mpango wa TASAF III  kunusuru kaya maskini 438 za wakazi wa kijiji cha Iguguno wilayani Mkalama.

Amesema watoto waliopo kwenye kaya maskini ndio wenye nafasi kubwa au uwezo wa kuweza kuzikomboa kaya hizo kwenye umaskini uliokithiri.

“Ninyi walengwa mnaopata ruzuku hakikisheni hizo fedha zinagharamia masomo ya watoto wenu na si vinginevyo.Tunataraji hizi ruzuku zisaidie, ili mwisho wa siku kila kaya iwe na mtoto mwenye elimu bora itakayowasaidia kumudu maisha yao na ya familia zao”,amesisitiza Dkt. Lutambi.

Aidha amezitaka kaya hizo kutumia ruzuku za huduma za afya kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF) ili kuwa na uhakika wa matibabu wakati wote hata kipindi hawana fedha.

“Kwa ujumla hizi ruzuku mnazopata kwa ajili ya kaya maskini mzitumie vizuri kwa malengo yaliyokusudiwa likiwemo la kujiongezea kipato na kujiunga na CHF. Msithubutu kuzitumia kunywea pombe zitumieni kwa kuanzisha miradi ya ufugaji kuku au mifugo”, amesema.

Kwa upande wake Mratibu wa TASAF Mkoani  Singida Patrick Kasang amesema kuwa kuanzia septemba 2014 hadi Julai mwaka huu, shilingi milioni 186,192,540 zimegawiwa kwa kaya maskini katika kijiji cha Iguguno.

“Na leo hii ndugu mgeni rasm jumla ya walengwa 438 walioko kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini hapa katika kijiji cha Iguguno watalipwa shilingi  milioni 15,516,045”, amesema Kasango. 
 
Kasango ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kutokana na ruzuku za mpango wa TASAF III kuwa ni ongezeko la mahudhurio ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambalo limechangiwa na wanafunzi kununuliwa sare na kupatiwa chakula cha mchana.

“Pamoja na ahadi ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John P. Magufuli ya elimu bure pia mpango wa TASAF III nao una mchango wake katika ongezeko la uandikishaji wa manafunzi kutoka 43,982 mwaka jana hadi wanafunzi 63,083 walioandikishwa katika mwaka huu”, amesema Kasango.

Amesema kupitia mpango huo jumla ya shilingi milioni 459.4 zimetumika kugharamia ujenzi wa zahanati nne na nyumba mbili za walimu katika vijiji tofauti Mkoani hapa.

Wakati huo huo, mkazi wa kijiji cha Iguguno Neema Zakaria ametumia fursa hiyo kuipongeza serikali kwa msaada unaoutoa kupitia TASAF III na kudai kuwa zimemsaidia kujenga nyumba bora ndogo ya bati na hivyo kuondokana na maisha ya kuishi kwenye nyumba ya tembe.

Ameongeza kuwa kabla ya kaya yake kuingizwa katika Mpango wa Tasaf yeye na familia yake hasa watoto walikuwa wakilala chini na hivyo pesa za tasaf licha ya kumsaidia mahitaji ya shule, afya na chakula ameweza pia kunua kitanda na kuwaepusaha watoto wake adha ya kulala chini.
Bi. Neema Zakaria Mkazi wa Kijiji cha Iguguno akitoa ushuhuda juu ya mafanikio aliyopata baada ya kuingizwa katika mpango wa Tasaf IIII.


Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina M. Lutambi akishiriki zoezi la kuhaulisha fedha kwa walengwa wa Tasaf kijiji cha Iguguno Wilayani Mkalama.

No comments:

Post a Comment