Wednesday, January 09, 2019

SERIKALI MKOANI SINGIDA, IMEAGIZA WANAFUNZI WOTE WALIOFAULU NA KUCHAGULIWA KUINGIA KIDATO CHA KWANZA MWAKA 2019 WAHAKIKISHE WANARIPOTI KWA WAKATI KATIKA SHULE ZAO WALIZOPANGIWA HATA KAMA HAWANA SARE ZA SHULE.

Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi, amesema cha kuzingatia zaidi ni mwanafunzi awe  na madaftari  na kalamu.
Dkt. Nchimbi ametoa agizo hilo hivi karibuni wakati akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya meza na viti kwa shule za Sekondari kutoka halmashauri ya wilaya ya Ikungi kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 2019. Hafla hiyo imefanyika kwenye viwanja vya shule ya Sekondari ya kata ya Ikungi.
Amesema kuwa, haamini kama kuna mzazi au mlezi yeyote atakayeshindwa  kumudu kununua sare ya mtoto wake. Amedai kuwa, kwa mkoa wa Singida unavyosifika kwa ufugaji wa kuku mzazi au mlezi akiuza kuku watatu tu wa kienyeji (akiwaita kuku wa Singida), atanunua sare na kubakiwa na chenji.
“Mtoto (mwanafunzi) atakayekosa sare, basi nguo atakazoenda nazo shule ziwe na hadhi ya shule (nguo zenye maadili ya shule), zisiwe zile ambazo zitamkosesha amani mtoto. Zikiwa choka mbaya, zitamchanganya kisaikolojia mwanafunzi na hivyo hatofanya vizuri kwenye masomo yake”, Amesema Dkt. Nchimbi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi, amesema kuwa, wanatarajia  kutumia zaidi ya shilingi 29.9 milioni, kwaajili ya kugharamia utengenezaji wa meza 700 na viti 700.
Alisema fedha hizo zinatokana na mapato ya ndani ya halmashauri hiyo na pia kutoka kwenye Mfuko wa Jimbo.
Kijazi amesema lengo la kutengeneza meza na viti hivyo ni wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu (2019), wanaingia madarasani.
Akisisitiza zaidi, mkurugenzi mtendaji huyo amesema, utengenezaji wa meza na viti hivyo ni mikakati waliojiwekea kuhakikisha wanafunzi  wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ndani ya halmashauri ya wilaya ya Ikungi wajiunge na shule walizochaguliwa bila kuwa na vikwazo.
Bw. Kijazi ameeleza kuwa, jumla ya  wanafunzi 1,572 wamemaliza kidato cha nne mwaka jana, na wanaotarajia kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu ni 4,690.
“Kuna ongezeko la wanafunzi 2,118. Ongezeko hili la wanafunzi limepelekea upungufu wa vyumba vya madarasa 23 vitakavyokidhi wanafunzi 376. Ongezeko hilo vile vile  limesababisha upungufu wa viti 2,118 na meza 2,118”, Kijazi alifafanua zaidi.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Bw. Kijazi amesema, Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa kutumia mapato ya ndani pamoja na fedha za Mfuko wa Jimbo la Magharibi inatengeneza jumla ya viti 700 na meza 700.
Hivyo katika awamu hii ya kwanza, Halmashauri imetengeneza viti 600 na meza 600 kwa kutumia mbao 542 zilizopatikana msituni kwa wavunaji haramu, mbao za kununua pamoja na fedha taslimu kutoka mapato ya ndani shilingi 19,935,000/= na fedha za mfuko wa jimbo la Magharibi shilingi 10,000,000/=, hivyo kufanya jumla ya fedha zote ni shilingi 29,935,000/=. Kwa sasa halmashauri ya wilaya imeanza kukamilisha meza 100 na viti 100 ili kukamilisha utengenezaji wa meza 700 na viti 700.
Aidha, Kijazi  amesema kila Kata inaendelea kutengeneza meza na viti kwa mujibu wa mahitaji ya shule zilizopo katika Kata hizo. Hadi sasa jumla ya meza 497 na viti 636 zimekwishatengenezwa.
“Hivyo, kila Mtoto (mwanafunzi) aliyefaulu kujiunga na masomo ya Sekondari 2019 atakuwa ameenda shule ambako atakuta KITI na MEZA na hivyo kusoma bila ya kikwazo chochote. Ni matarajio yetu kuwa kwa shule ambako bado kuna changamoto chache zilizobaki watakamilishiwa kwa muda mfupi” Amesema Bw. Kijazi.
Wakati huo huo, mkuu wa wilaya ya Ikungi, Miraji Mtaturu, alisema ofisi yake inafuatilia kwa karibu sekta ya elimu na hasa kipindi hiki shule zinapofunguliwa.
KATIKA HATUA NYINGINE
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi, amesikitishwa na taarifa ya Fedha za Mfuko wa Jimbo la Singida Mashariki kutokumika kikamilifu katika kuleta maendeleo ya wananchi wa maeneo husika hali iliyompelekea kulikemea vikali jambo hilo linalofanywa na baadhi ya viongozi wa Jimbo la Singida Mashariki.

“Fedha za Mfuko wa Jimbo ni mali ya Serikali, Fedha za mfuko wa Jimbo ni mali ya wananchi, Fedha za Mfuko wa Jimbo ni kwa manufaa ya wananchi. Kifanywe kinachofanyika kwa namna yoyote ile, fedha za mfuko wa Jimbo zionekane na zidhihirike zinatumika kwa maslayi ya wananchi na kwa maslayi ya umma”.

“Hatuwezi kukubali kuendelea hivi tunavyoendelea, kama mtu anataka kufanya mzaha na mchezo na fedha, afanye mzaha na mchezo na fedha zake binafsi lakini sio fedha za Umma”.

“Ninaomba viongozi wa Dini na Madhehebu wa Ikungi, tusaidiane katika hili, katika Dini na Madhehebu hakuna siasa, hakuna uvyama, na tumeambiwa maendeleo hayana chama. Mheshimiwa Rais anasimamia vyama vyote na maendeleo ni kwa wananchi wa vyama vyote. Haiwezekani swala la imani ya chama ikawa kikwazo kwa maendeleo yetu".

“Katika mkoa wangu (Singida) na katika uongozi wangu kunalimzigo hili la kutokuwa na matumizi sahihi ya fedha za mfuko wa Jimbo la Singida Mashariki. Tunataka mfuko wa Jimbo utumike unavyotakiwa kutumika, ninataka mfuko huu haraka sana utumike kwa kutatua changamoto za madawati".

"Fedha zile si za mtu binafsi, fedha zile ni kwa maslayi ya wananchi wa Jimbo la Singida Mashariki” Amesema Dkt Nchimbi.

Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya Ikungi, Mhe. Juma Mwanga, amesema amefurahishwa na mkuu wa mkoa Dkt. Nchimbi kwa kutambua tatizo hilo la mfuko wa Jimbo la Singida Mashariki kutokutumika kwa mambo yaliyokusudiwa.

“Mkuu wa mkoa, wilaya yetu ina majimbo mawili, tuna Jimbo la Singida Mashariki na Jimbo la Singida Magharibi. Mfuko wa Jimbo la Singida Magharibi hatuna tatizo na fedha za mfuko wa Jimbo hilo. Fedha zikija zinatumika kwa wakati na kwa matumizi ya maendeleo. Shida ipo katika fedha za Mfuko wa Jimbo la Singida Mashariki”,

 Tunatumia nguvu nyingi kumshawishi mwenyekiti wa mfuko kuwa fedha hizo zitumike kwa maendeleo ya wananchi lakini huwa hatuelewi kabisa. Ipo siku alisema fedha hizo anazielekeza kununua chakula cha msaada kwa baadhi ya wapiga kura wake”. Amesema Mhe. Juma Mwanga.
MATUKIO KATIKA PICHA



Mkuu wa wilaya ya Ikungi Mheshimiwa Jumanne Mtaturu akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya meza na viti kwa shule za Sekondari kutoka halmashauri ya wilaya ya Ikungi kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 2019.


Mkuu wa wmkoa wa Singida akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya meza na viti kwa shule za Sekondari kutoka halmashauri ya wilaya ya Ikungi kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 2019.


Wanafunzi kutoka shule mbalimbali za sekondari halmashauri ya wilaya ya Ikungi walioshiriki katika hafla ya makabidhiano ya meza na viti kwa shule za Sekondari kutoka halmashauri ya wilaya ya Ikungi kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 2019.

Mkuu wa wilaya ya Ikungi Mheshimiwa Jumanne Mtaturu akielezea jambo wakati wa zoezi la kukagua meza na viti katika hafla ya makabidhiano ya meza na viti kwa shule za Sekondari kutoka halmashauri ya wilaya ya Ikungi kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 2019.



Afisa Elimu mkoa wa Singida Mwalimu Elasi Mulungu (wa tatu kutoka kulia) pamoja na watendaji wengine wa halmashauri ya wilaya ya Ikungi, wakishuhudia meza na viti vilivyotengenezwa na halmashauri ya wilaya ya Ikungu kwa ajili ya kukabidhi kwa shule za Sekondari kutoka halmashauri ya wilaya ya Ikungi kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 2019.




Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akikabidhi meza na viti kwa shule za Sekondark kutoka halmashauri ya wilaya ya Ikungi kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 2019.






 Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akiwa na wanafunzi mbalimbali wa sekondari za halmashauri ya wilaya ya Ikungi, wakionyesha ishara ya kidole kimoja huku wakisema "SISI NI WA DIVISION ONE". 



 Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi pamoja na Mkuu wa wilaya ya Ikungi Mheshimiwa Jumanne Mtaturu akikabidhi mizinga ya nyuki kwa baadhi ya Walimu walioshiriki kwenye hafla ya makabidhiano ya meza na viti kwa shule za Sekondari kutoka halmashauri ya wilaya ya Ikungi kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 2019. Mizinga hiyo ni kwaajili ya kutekeleza kampeni ya mkuu wa mkoa huyo ya kutunza mazingira katika mkoa na halmashauri hiyo kwa kauli mbiu ya ACHIA SHOKA KAMATA MZINGA. 





 Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi pamoja na Mkuu wa wilaya ya Ikungi Mheshimiwa Jumanne Mtaturu na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi Bw. Justice Kijazi wakiwa katika picha ya pamoja ya kutakiana kheri ya mwaka mpya (cheers) na baadhi ya Walimu walioshiriki kwenye hafla ya makabidhiano ya meza na viti kwa shule za Sekondari kutoka halmashauri ya wilaya ya Ikungi kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 2019. Hafla hiyo imefanyika kwenye viwanja vya shule ya Sekondari ya kata ya Ikungi.

IMETOLEWA NA;
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO 
OFISI YA MKUU WA MKOA 
SINGIDA

No comments:

Post a Comment