Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko ameuagiza Mgodi wa Dhahabu wa Shanta uliopo katika wilaya
ya Ikungi mkoani Singida kuhakikisha unatoa taarifa za tafiti zake
zilizofanyika katika maeneo mbalimbali ili wachimbaji wadogo waweze kuzitumia
katika kubaini madini yaliyopo na kuanza kuchimba kwa kufuata sheria na kanuni
za madini.
Naibu Waziri Biteko
alitoa agizo hilo tarehe 19 Novemba 2018 kwenye mkutano wa hadhara na
wachimbaji wadogo wa madini uliofanyika katika tarafa ya Mang’onyi wilayani
Ikungi mkoani Singida kama sehemu ya ziara yake katika mkoa huo yenye lengo la
kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wachimbaji wa madini.
Aliongeza kuwa
Serikali kupitia Wizara ya Madini imeweka mazingira bora ya uchimbaji wa madini kwa wachimbaji wadogo ikiwa ni
pamoja na kuwapatia taarifa mbalimbali
za utafiti zilizofanywa na Wakala wa Utafiti na Jiolojia Tanzania (GST)
na kampuni za utafiti wa madini lengo
likiwa ni kuhakikisha kuwa uchimbaji wao unakuwa wa
uhakika na sio wa kubahatisha.
Akielezea maboresho
mengine yaliyofanywa katika sekta ya madini, Biteko alisema Serikali
imeboresha Sheria ya Madini inayotambua
madini kama mali ya watanzania yanayosimamiwa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
Aliendelea kusema
kuwa, Serikali imeweka mkakati wa kurasimisha wachimbaji wadogo wa madini wasio
rasmi na kuwapatia leseni za madini ili
uchimbaji wao ulete tija kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.
Katika hatua nyingine,
Naibu Waziri Biteko aliwataka wachimbaji wadogo wa madini kuunda vikundi na
kupewa leseni ili waanze kuchimba na
kulipa kodi Serikalini.
“Sisi kama Serikali
kupitia Wizara ya Madini lengo letu ni kuhakikisha kuwa tunaweka mazingira bora
kwa wachimbaji wadogo wa madini ili uchimbaji uongeze kasi ya ukuaji wa uchumi
kupitia kodi na tozo mbalimbali,” alisema Biteko.
Wakati huohuo Biteko
aliwataka wananchi wanaoishi karibu na Mgodi wa Dhahabu wa Shanta kutokuharibu
miundombinu ya maji iliyowekwa ili iweze
kunufaisha wananchi wote.
Awali wakiwasilisha kero
mbalimbali wakazi hao waliiomba Wizara ya Madini kuwapatia maeneo kwa ajili ya
uchimbaji wa madini ili waweze kujiingizia kipato na kulipa kodi Serikalini.
Akizungumza kwa niaba
ya wachimbaji wadogo wa madini katika tarafa ya Mang’onyi iliyopo wilayani
Ikungi mkoani Singida, Consolata Joseph alisema kuwa uchimbaji wao umekuwa ni wa kubahatisha na hata kuvamia
maeneo yenye leseni kubwa ya madini inayomilikiwa na Kampuni ya Dhahabu ya
Shanta.
Awali akizungumza
katika ziara hiyo, Meneja Mkuu wa Mgodi
wa Dhahabu wa Shanta uliopo wilayani Ikungi mkoani Singida, Philbert Rweyemamu
alisema mgodi umeshaanza kutoa fidia na kuongeza kuwa mpaka sasa umeshatoa
shilingi bilioni 2.6 pamoja na ujenzi wa makazi mbadala ambapo mpaka sasa
wameshajenga nyumba sita.
Aliongeza kuwa mpaka
ifikapo mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu, mgodi unatarajia kukamilisha
ujenzi wa nyumba nyingine sita na kufanya idadi ya nyumba kuwa 12 kama sehemu
ya kuhakikisha wananchi wanaolipwa fidia wanaishi katika mazingira mazuri.
Akizungumzia
changamoto za mgodi wake, Rweyemamu alieleza kuwa ni pamoja na wachimbaji
wadogo haramu kuvamia eneo la mgodi na
kuchimba madini, miundombinu kuhujumiwa na baadhi ya wananchi kugomea fidia
inayotolewa na kampuni hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Ikungi Mhe. Miraji J. Mtaturu akizungumza.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati) akiangalia makubaliano ya maandishi yaliyofanywa kati ya mmiliki wa kampuni inayojishughulisha na uchimbaji wa madini ya jasi ya General Business and Equipment Supply Limited.
Uchimbaji wa madini ya jasi ukiendelea katika eneo la kampuni ya General Business and Equipment Supply Limited iliyopo katika eneo la Bumbua wilayani Itigi mkoani Singida.
HABARI NA MAWASILIANO
OFISI YA MKUU WA MKOA
SINGIDA
No comments:
Post a Comment