Tuesday, November 13, 2018

MKOA WA SINGIDA WAANZA KUCHUKUA HATUA KATIKA KUKABILIANA NA HALI DUNI YA LISHE KWA WATOTO CHINI YA UMRI WA MIAKA MITANO.


  Mkuu wa Mkoa SINGIDA DKT. REHEMA NCHIMBI ameziagiza halmashauri zote za mkoa wa SINGIDA zihakikishe zinatenga bajeti ya mwaka wa fedha wa 2019/2020 kwa ajili ya masuala ya LISHE kwa kutumia mapato ya ndani kama hatua ya kukabiliana na hali ya udumavu hasa kwa watoto wenye umri chini ya miaka MITANO na wanawake wenye umri kati ya 15- 49.

Mkuu huyo wa mkoa wa Singida ametoa maagizo hayo mjini hapa, tarehe 12/11/2018 katika kikao kazi kuhusu ujumuishwaji wa afua za lishe katika mipango ya bajeti za mikoa na halmashauri kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.

Dkt. Nchimbi amesisitiza kuwa lishe bora katika jamii ni kichocheo cha maendeleo katika nyanja zote kama vile afya, kilimo, elimu, biashara na uchumi.

Ameeleza kuwa athari za lishe duni au utapiamlo zitakapodhibitiwa au kutokomezwa ndipo malengo ya maendeleo katika nyanja mbalimbali Kimkoa na Kitaifa zitaweza kufanikiwa kikamilifu.

Aidha amefafanua kuwa jambo la msingi ambalo wataalamu na jamii wanapaswa kulifahamu na kulizingatia ni ukweli kwamba lishe ni suala mtambuka na utapiamlo katika jamii ni matokeo ya mkusanyiko wa matatizo mengi.

Ametaja baadhi ya matatizo hayo kuwa ni mtindo wa maisha usiofaa, maradhi mbalimbali, kutokuwa na uhakika wa chakula, matunzo duni ya mama na watoto, mazingira machafu, umaskini wa kipato na machafuko ya kisiasa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TAMISEMI Bi. BEATRICE KIMOLETA akizungumza katika kikao hicho amekiri kuwa hali ya lishe katika baadhi ya mikoa nchini sio nzuri hivyo jitihada za makusudi zinatakiwa ili kuhakikisha tatizo hilo linakoma hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchumi wa kati wa viwanda.

Mkurugenzi huyo pia ameagiza masuala ya lishe yajadiliwe kwa kina katika vikao vyovyote vya maendeleo ngazi zote na kuhimiza ushirikishaji wa maafisa lishe katika ngazi za uandaaji wa bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe.

MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI KIKAO KIKIENDELEA








 
  

 


 
 


IMETOLEWA NA;
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO
OFISI YA MKUU WA MKOA
SINGIDA

No comments:

Post a Comment