Tuesday, October 23, 2018

DKT. HUSSEIN MWINYI ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA UJENZI INAYOTEKELEZWA NA SUMA JKT MKOANI SINGIDA



Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. HUSSEIN MWINYI amewagiza watendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa - SUMA JKT - kukamilisha ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotelezwa na shirika hilo kwa viwango vinavyotakiwa ili majengo hayo yaanze kutumika haraka kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi kwa muda muafaka.

Waziri Dkt. Mwinyi ametoa kauli hiyo mjini Singida wakati akikagua miradi inayotekelezwa na SUMA JKT ikiwemo ukarabati wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Singida, ujenzi wa nyumba ya mganga mkuu wa mkoa wa Singida na Ujenzi wa Jengo la Kuhifadhi Maiti katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida iliyopo Mandewa na kuonyesha kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo. 

"Nimeridhika kwa kiwango kikubwa na kiwango cha ujenzi na spidi inayoendelea na washitili  wetu ambao ni mkoa nao wameridhika kwa hatua nzuri za ujenzi zinavyokwenda vizuri na kwa kiwango kizuri, kwahiyo tunashukuru kwahilo. Lakini nia na madhumini ya ziara hii ni kuja kuangalia kwa ujumla kazi zinazofanywa na kampuni yetu ya SUMA na kiwango cha kazi wanazozifanya pamoja na endapo washitili (wateja) wetu wanaridhika na kazi zetu ili tuweze kutatua zile changamoto ambazo zinawakabili na kama kuna mafanikio basi  tuweze kuyakuza zaidi katika maeneo mbalimbali" Dkt. Mwinyi.

Waziri Dkt. HUSSEIN MWINYI amesisitiza kuwa Wizara hiyo kwa ushirikiano na Watendaji wa SUMA JKT wataendelea kuondoa changamoto mbalimbali zinazojitokeza ili kuhakikisha ujenzi wa miradi hiyo unakamilika kwa wakati unatakiwa bila kuchelewa.
  
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa mkoa wa SINGIDA Dkt. ANGELINA LUTAMBI amesema Serikali ya mkoa Singida imeamua kulipatia Shirika la SUMA JKT zabuni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kutokana na kasi na ubora wa utekelezaji wa miradi kulingana na thamani ya fedha inayotolewa na Serikali.


Shirika la SUMA JKT kwa mkoa wa SINGIDA linatekeleza miradi 12 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 2.5 

MATUKIO KATIKA PICHA


 

  




 

 
   


 



 IMETOLEWA NA;
KITENGO CHA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO
OFISI YA MKUU WA MKOA 
SINGIDA

No comments:

Post a Comment